Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya, Rigathi Gachagua amezungumza kuhusu sababu za kukosa baadhi ya matukio muhimu ya kitaifa ambayo yanahudhuriwa na maafisa wa serikali pamoja na Rais William Ruto.
Akizungumza jana Ijumaa katika mahojiano na Citizen TV, Gachagua amefichua kwamba yeye na timu yake wameondolewa kwenye kundi la WhatsApp ambamo huwekwa ratiba ya rais, labda kwa lengo la kuwafanya washindwe kushiriki masuala ya kitaifa.
Amedai kuwa Katibu binafsi wa Rais, Reuben Miayo, aliondoa timu yake kutoka kwenye ratiba ya Rais wiki moja iliyopita, na hivyo amekuwa hajui kinachoendelea na hawezi kuhudhuria hafla za mkuu wa nchi.
"Takriban wiki moja iliyopita, tuliondolewa kwenye hiyo ratiba hivyo hatukuwa tunaweza kufuatilia kinachoendelea na kwa hivyo hatuwezi kujiunga. Ninapojua mahali Rais yupo, mimi huwa hapo. Nikikosa kujua, sina la kufanya," amesema Gachagua.
"Ni katika kundi la WhatsApp tunajua ratiba za kila siku. Lakini niliondolewa mimi, katibu wangu binafsi na mkuu wa wafanyakazi (kwenye ofisi yangu), kwa hivyo hatujui ratiba ya Rais."
Amesema kuwa kuondolewa huko anahisi kunalenga kuhakikisha kwamba anashindwa kuhudhuria hafla za kitaifa au afike akiwa amechelewa ili aonekane kama asiyeheshimu au anayekwepa majukumu yake.
Gachagua ameiomba Ofisi ya Rais na wale wanaohusika waruhusu timu yake kujumuishwa kwenye ratiba za Rais, akisisitiza nafasi yake kama mtu wa pili kwa mamlaka ya nchi ili atimize majukumu yake kwa wananchi.
Chanzo: Citizen TV