Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde amezindua ujenzi wa jengo la mapumziko la wananchi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kusema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utatuzi wa changamoto zinzazowakabili wananchi.
Mavunde amesema kuwa nje ya jengo hilo kuna eneo ambalo wanakaa wananchi ambao asilimia kubwa hawaishi katika Jiji la Dodoma na wanatumia sehemu ile kama sehemu ya kupumzikia kwa ajili ya kusubiri muda wa kuwaona wagonjwa wao.
Ameongeza ujenzi wa Jengo hilo ni muhimu kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawana sehemu ya kulala na hawana makazi Dodoma na hawawezi kurudi walipotoka kwasababu ya umbali na gharama za usafiri.
Kwa mujibu wa mbunge huyo ambaye pia ni Waziri wa Madini kuna wakati mwingine wakina mama,baba na watoto wanachanganyikana na kulala sehemu moja.
"kulingana na maadili ya kitanzania sio vema sana kuchanganyika watu wa jinsi tofauti sehemu moja na hasa ambao kwa namna moja au nyingine hawana uhusiano wowote. jambo hili lilinigusa sana nikasema moja ya sadaka, Mungu akinijalia na nitapenda niiache kama alama ni kuwahifadhi na kuwasitiri wananchi wangu ambao wanakaa katika eneo lile ambalo lipo wazi"alisema Mavunde na kuongeza kuwa
"Nilisema nitalifanyia kazi na leo ndugu zangu nimezinduaa rasmi ujenzi wa jengo la kisasa kabisa na wananchi wa ndani na nje ya Dodoma watapata sehemu nzuri ya kupumzika"
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt.Sarah Ludovick akitoa taarifa fupi kuhusu hospitali hiyo, amebainisha changamoto mbalimbalo wanazopitia katika baadhi ya majengo yanayotoa huduma hospitalini hapo.
Dkt.Ludovick amesema kuwa hospitali hiyo ina miaka 104 na ilianza kama kituo cha afya na imekua na kufikia hadhi ya kuwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo ametumia fursa hiyo kumshukuru Mbunge Mavunde kwa moyo wake wa kutatua moja ya changamoto iliyokuwa inawakabili wananchi.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa CCM Wilaya Charles Mamba amepongeza hatua ya ujenzi wa jengo la kupumzikia wananchi na kusema kuwa CCM inaunga mkono jitihada zinazofanywa na Mbunge Mavunde katika kuhudumia wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Dodoma Legends Ahmad Toufiq ameeeleza kufurahishwa na kazi kubwa anayoifanya Mbunge Mavunde na kuchangia mifuko 100 ya saruji kuunga mkono Juhudi za mbunge hiyo.