Na Lubango Mleka, Igunga.
WANACHAMA na Mashabiki wa Timu ya Yanga Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wameadhimisha wiki ya Mwananchi kwa kutembelea wodi ya Watoto katika Hospitali ya wilaya ya Igunga na Gereza la Wilaya ya Igunga na kutoa mahitaji mbalimbali.
Kilele hicho kimeanza kwa maandamano ya amani kutokea uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine uliopo Mamlaka ya mji mdogo wa Igunga na kuelekea katika Hospitali ya wilaya ya Igunga na kuwafariji Wazazi na Watoto ambao ni wagonjwa kwa kuwapatia juisi, maji ya kunywa, sabuni za unga na vipande, dawa za miswaki, mafuta pamoja na pampasi.
Wamehitimisha maadhimisho hayo kwa kutembelea Gereza kuu wilaya ya Igunga ambapo wametoa kiasi cha sh. 30,000 kwa ajili ya kununua kifurushi cha Azam ili Wafungwa na Mahabusu wapete fursa ya kufuatilia kilele cha wiki ya Mwananchi, aidha wametoa sabuni za unga na vipande, viwembe, maji ya kunywa na mipira miwili kwa ajili ya kufanya mazoezi.
Mkaguzi Msaidi I. R. Ntandu kwa niaba ya Mkuu wa gereza la wilaya ya Igunga amewashukuru Wanachama wa Yanga wilayani hapa kwa kuguswa na kukumbuka kuwa kuna watu ambao ni miongoni mwajamii wanaohitaji faraja kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na kuwapatia mipira na kuwanunulia kifurushi kwa ajili ya kufuatilia taarifa mbalimbali za habari na michezo.
Huku mmoja ya wazazi ambaye mtoto wake amelazwa wodi namba 9 katika Hospitali ya wilaya ya Igunga, Jacline Dickson akisema, " Tunawashukuru Timu ya Wananchi kwa kutukumbuka kwani hiki mlichokifanya ni zaidi ya timu, mmetutembelea na kukumbuka watoto wetu wagonjwa, na hii ni neema ya kipekee sana kwetu na muendelee kufanya makubwa tumefurahi sana. "
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Lucia Kafumu, Muuguzi Msaidizi Nyasatu Daniel amewapongeza Wananchama hao kwa kuwiwa na kuwajali watoto ambao ni wagonjwa hivyo kuwaomba kujitoa zaidi kwa kurudisha fadhila kwa jamii kwani michezo ni amani na furaha hivyo wameonesha furaha kwa Wazazi na Watoto wao kuwa wapo pamoja katika kurudisha furaha ya watoto wao ambao ni wagonjwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tawi la Yanga Bingwa Igunga Mjini Paul Mtani akisema kuwa wameguswa kurejesha fadhira kwa wahitaji hivyo wameona ni vyema kuwatembelea watoto na wafungwa na mahabusu kwani ndio kundi ambalo tumeona linauhitaji mkubwa sana, hivyo kwa hicho kidogo ndicho walicho anzia na wameahidi kuendelea kutoa zaidi kwa waitaji wengine ambao hawajafikiwa leo.




Comments
Post a Comment