Shirikisho la soka Tanzania limekabidhi mipira mia tano kwa jeshi la ulinzi wa wananchi Tanzania JWTZ, kwa ajili ya kuendeleza michezo kwa vijana wenye umri kati ya miaka sita hadi kumi na nne, kupitia vituo maalumu vya mafunzo ya michezo vinavyo tarajia kuanzishwa na JWTZ.
Akikabidhi sehemu ya mipira mia tano kwa mkuu wa majeshi ya ulinzi ya wananchi wa Tanzania, Rais wa TFF Wallace Karia, amesema TFF imetoa mipira hiyo katika kutekeleza ahadi yake ya kulisaidia jeshi katika sekta ya michezo hasa wa mpira wa miguu.
Karia ambaye ameambatana na maafisa mbalimbali wa TFF, pamoja na kulipongeza Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania katika kuendeleza mpira wa miguu nchini, amemuomba mkuu huyo wa Majeshi kufikiria kuanzisha timu za mpira wa miguu za ufukweni (beach soka) ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa.
Hata hivyo pamoja na kupongeza jeshi kwa mpango wake wa ujenzi wa vituo hivyo vya mafunzo ya michezo,amesema kuwa huwezi kutaja mpira wa Tanzania bila kulitaja Jeshi hasa kwa timu za wanawake kupitia JKT .
Ameliomba Jeshi katika progaramu yake ya ukarabati wa viwanja vyake pia waangalie uwezekano wa kukarabati uwanja wa Lake Tanganyika, unaotumiwa na timu ya Mashujaa inayoshiriki ligi kuu nchini.
Nae mkuu wa Majeshi ya ulinzi nchini Jenerali Jacob John Mkunda, akizungumza baada ya kupokea mipira hiyo pamoja na kushukuru TFF kwa kutekeleza ahadi hiyo,ameiomba TFF kuendelea zaidi kulisaidia jeshi kwenye sekta ya michezo.
Amesema michezo ni sehemu na kazi ndani ya Jeshi, hivyo kumekuwa na juhudi kubwa za kuinua sekta ya michezo ukiwemo mpira ya miguu.
Mkuu hiyo wa majeshi nchini,ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan. kwa moyo wake wa kupenda michezo na kulisaidia Jeshi hilo.
Amesema Watanzania wameshuhudia hamasa kubwa inayofanywa na mkuu huyo wa nchi katika sekta ya michezo na kwamba Jeshi tayari limetambua juhudi hizo za mh Rais na kuiomba TFF na wadau wengine waunge mkono juhudi hizo.
Hafla hiyo fupi imeshirikisha maafisa mbalimbali wa vyeo vya ngazi ya juu ya Jeshi la ulinzi la wananchi Tanzania, akiwemo mkuu wa oparesheni na mafunzo jeshini meja jenerali Ibrahim Mhona na mkuu wa tawi la Utawala wa JKT Bridia Jenerali Hassan Mabena.









.jpg)





Comments
Post a Comment