Na George Marato-Mapinga
WAZIRI wa ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dtk Stergomena Lawrence Tax amesema Tanzania itaendeleza mahusiano na nchi rafiki ikiwemo China katika kuimarisha Diplomasia ya ulinzi ili kuongeza uwezo kwa jeshi la Ulinzi la Wananchi katika kukabiliana na matukio mbalimbali ya matishio ya amani duniani.
Akizungumza wakati wa kufunga zoezi la Medani la ushirikiano wa miaka 60 kati ya JWTZ na jeshi la ukombozi la watu wa China,waziri huyo wa Ulinzi na JKT,mbali na kumpongeza Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia zoezi hilo kufanyika hapa nchini,amesema zoezi hilo linaimarisha ushirikiano na undugu kwa mataifa haya mawili.
Amesema Tanzania na China zina historia kubwa kimahusiano na kwamba mahusiano hayo kwa sasa yako kwenye hali ya juu,lakini pia zoezi hilo la medani kwa kuhusisha majeshi ya nchi hizi mbili,limewezesha kubadilisha ujuzi na kuimarisha kwa kiasi kikubwa sekta yetu ya ulinzi kwa JWTZ.
Katika salamu zake kwa jeshi la ulinzi wa Wananchi Tanzania ambazo zimetolewa na waziri huyo wa ulinzi na JKT, Rais Samia Suluhu Hassan,amesema anajivunia kwa kiasi kikuwa kuwa na jeshi lenye ueledi wa hali ya juu,na kwamba amesema Serikali itafanya kila liwezekanalo katika kulisaidia jeshi kwa nyanja zote zikiwemo za kimafunzo.
Kwa upande wake mkuu wa majeshi ya ulinzi Generali Jocob John Mkunda,amesema utashi wa Rais Samia Suluhu Hassan, umewezesha jeshi hilo kuwa na vifaa vya kisasa na uwezo mkubwa.
Mkuu huyo wa Majeshi ametumia nafasi hiyo kumpongeza Amri jeshi mkuu Rais Samia,kwa kuliwezesha jeshi hilo kuwa na vifaa vya kisasa na hivyo kuleta mabadiliko makubwa ndani ya jeshi.
Hata hivyo amesema kufanyika kwa zoezi hilo la pamoja kati ya Tanzania na China,limewezesha jeshi kujitathimini kiuwezo na kwamba limewezesha pia kuongeza hamasa kubwa askari na wapiganaji ambao wameshiriki katika zoezi hilo.
Waziri huyo wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa,pamoja na waambata wa kijeshi wa nchi rafiki, wameshuhudia zoezi la kulenga shabaha,zoezi la kukabiliana magaidi, ambalo limehusisha vikundi vya askari wa Tanzania na China.
Jeshi la Ukombozi la watu wa China,limeshiriki zoezi hilo la shamrashamra ya miaka 60 ya kuzaliwa kwa JWTZ hapo septemba 01 mwaka huu,ambapo walishiriki kutoa matibabu bure kwa Watanzania na kushiriki katika zoezi hilo la medani.




.jpg)
.jpg)









Comments
Post a Comment