JESHI la ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) linakusudia kuzindua mashindano yanayolenga kuhuisha Sanaa, na muziki wa dansi wenye asili ya kitanzania na Africa.
Uamuzi huo wa JWTZ umechukuliwa baada ya kubaini kuanza kusahaulika kwa Sanaa hiyo na kwamba mashindano hayo yatawezesha watanzania kujivunia utamaduni wao, na kuleta mabadiliko makubwa ya kimaadili kwa Taifa.
Mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na Mkuu Wa Majeshi Jenerali Jacob John Mkunda, kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo ya muziki wa dansi na ngoma za asili, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy ,ametangaza uamuzi huo leo Agosti 10-2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa jeshi wa Msasani Club Jijini Dar es Salaam.
Amesema baada ya kuzorota kwa Sanaa hiyo hapa nchini, jeshi la ulinzi wa wananchi kupitia kwa mkuu wake wa majeshi,aliunda kamati kwa kushirikisha wadau mbalimbali ambayo pamoja na mambo mengine imeandaa mashindano hayo ili kuhuisha Sanaa hiyo nchini.
Meja jenearali Mkeremy,amesema kutokana na nia hiyo njema ya mkuu wa majeshi ya kuhuisha sanaa hiyo,jeshi litazindua mashindano hayo Augusti 19 mwaka huu, kwa kushirikisha Mziki wa Dansi na Vikundi vya Ngoma za asili kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amewaambia waandishi wa hao wa habari wakiwemo wajumbe wa kamati hiyo kuwa mashindano hayo ambayo pia ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya kuzaliwa kwa jeshi la ulinzi la wananchi Tanzania (JWTZ) kwa mwaka huu yatahusisha bendi kumi za mziki wa dansi na vikundi tisa vya ngoma za asili kutoka vikosi mbalimbali vya jeshi hilo.
Hata hivyo amesema kutokana na mafanikio ya mashindano hayo mwaka huu,mwaka kesho kuna uwezekano wa kushirikisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama yakiwemo Polisi,Uhamiaji na Magereza.
Amesema zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi watatu kwa kila eneo ikiwa ni pamoja na Sanaa zao kurekodiwa,huku akiwaomba wanchi kujitokeza kwa wingi wakati wa uzinduzi na wakati wote wa mashindano hayo kuanzia Agosti 19 hadi 30.
Amesema hakutakuwa na kiingilio na ulinzi utaimarishwa wa kuwezesha wananchi kushuhudia mashindano bila kusumbuliwa na kwamba huduma zote za vyakula na vinywaji zitapatikana hata kwa kutumia fukwe za eneo hilo kuogelea.
Waziri wa Utamaduni,Sanaa,na Michezo Damasi Ndumbaro, ndiye anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo huku waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Mhe. DKT Stergomena Lawrence Tax anatarajiwa kufunga mashindano hayo Agosti 30 mwaka huu.






Comments
Post a Comment