JESHI la ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) linakusudia kuzindua Mashindano yanayolenga kuhuisha Sanaa na muziki wa dansi wenye asili ya kitanzania na Africa ambao umeanza kusahaulika nchini, hatua ambayo itawezesha watanzania kujivunia utamaduni wao, na kuleta mabadiliko makubwa ya kimaadili kwa taifa.
Mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na Mkuu Wa Majeshi Jenerali Jacob John Mkunda, kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo ya muziki wa dansi na ngoma za asili, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy , amesema baada ya kuzorota kwa Sanaa hiyo hapa nchini, jeshi la ulinzi wa wananchi kupitia kwa mkuu wake wa majeshi, litazindua mashindano hayo August 19 mwaka huu, kwa kushirikisha Mziki wa Dansi na Vikundi vya Ngoma za asili kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.
Meja Jenerali Mkeremy, amewaambia waandishi wa habari kuwa mashindano hayo ambayo pia ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya kuzaliwa kwa jeshi la ulinzi la wananchi Tanzania (JWTZ), na kwamba kamati imebaini baadhi ya tamaduni na Sanaa zimeanza kupotea hapa nchini.
Kwa sababu hiyo, amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kushuhudia mashindano hayo yatakayozinduliwa na Waziri wa Utamaduni,Sanaa,na Michezo Damasi Ndumbaro, kwa kuhusisha bendi 10 za muziki wa dansi, na vikundi 9 vya ngoma za asili.



Comments
Post a Comment