Na Shomari Binda- Musoma
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma( MUWASA) imejipanga Kuongeza Huduma ya upatikanaji wa maji safi na Salama Kwa Wananchi Kupitia Mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji kwenye mitaa 7 ya pembezoni manispaa ya manispaa ya Musoma unakusudiwa kuhudumia watu 40,000.
Mitaa iliyopo kwenye mradi huo na watu wake kupata huduma hiyo ya maji ni Kwangwa A na B, Kiara, Songambele, Nyabisare, Bweri na Bweri Bukoba.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) Mhandisi Nicas Mugisha, wakati akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Godfrey Mnzava leo julai 30 ulipotembelea mradi huo.
Amesema mradi huo unaoghalimu kiasi cha milioni 600,000,000 ulianza novemba 2023 na unatarajiwa kukamilika novemba 2024.
Nicas amesema lengo la mradi ni kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi wa manispaa ya Musoma kutoka asilimia 95 na kufikia 98.
" Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge mradi huu utakapokamilika utahudumia watu 40,000 na utaongeza mtandao wa maji ya bomba.
Mapato yataongezeka kwa mamlaka na magonjwa ya mlipuko yatawaepuka wananchi kutokana na kupata maji safi na salama"Amesema.
Akizungumza kwenye mradi huo kiongozi wa mbio za mwenge Godfrey Mnzava amesema serikali inaendelea kufanya jitihada za kumtua mama ndoo kichwani.
Amesema miradi yote iendelee kusimamiwa na kukamilika kwa wakati kutokana na mikataba inavyoeleza ili wananchi wapate huduma.
Mwenge wa uhuru upo manispaa ya Musoma ukitembelea,kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo na baadae kuendelea na mbio zake halmashauri ya Musoma,Butiama na Bunda na kukabidhiwa mkoani Simiyu.


Comments
Post a Comment