Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, ameeleza kuwa Jamhuri ya Indonesia itaendelea kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.
Mhe. Nyongo amesema hayo, Julai 19, 2024, wakati Mhe.alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury, ambaye alifika nchini kuzungumza juu ya mashirikiano na Tanzania, miongoni mwa hayo ilikuwa ni kuikaribisha Tanzania kwenye Kongamano la Biashara kati ya Indonesia na nchi za Afrika (Indonesia - Africa Forum) linalitegema kufanyika 1-3 Septemba, 2024 nchini Indonesia
Mhe. Nyongo amethibitisha Tanzania kushiriki katika kongamano hilo na wamejadili masuala ya uwekezaji wa Indonesia katika sekta mbalimbali nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kilimo, nishati safi, mitandao, viwanda, na miundombinu.
Mhe. Nyongo aliongeza kuwa kampuni moja kutoka Indonesia ipo tayari kutekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa mbolea inayotokana na gesi hapa nchini, mradi ambao utakuwa na thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.2. Huu ni mfano wa dhamira ya Indonesia kuwekeza kwa kina katika sekta muhimu za Tanzania.
Kwa upande mwingine, Mhe. Mansury alisema kuwa Kongamano la Biashara limeandaliwa ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Indonesia na nchi za Afrika, hasa Tanzania. Alifafanua kwamba Indonesia Kongamano hilo litahusisha majadiliano kati ya mawaziri, wafanyabiashara wa Indonesia, na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.



Comments
Post a Comment