Na Shomari Binda-Musoma
KATIKA kuongeza na kupata wana sayansi wengi kutoka Musoma vijijini shule zenye Kidato Cha Tano na Sita(A-Level) zinakusudiwa kuongezwa hasa zenye mchepuo wa masomo ya sayansi.
Kwa sasa sekondari ya Etaro inaendelea kuongezwa miundombinu ili kuifanya kuwa na Kidato Cha Tano na Sita ikikusudiwa kuwa na somo la kompyuta ya sayansi.
Kata ya Etaro yenye vijiji vinne (4) inayo sekondari moja iliyoko Kijijini Etaro na sekondari ya pili ya Kata hii inajengwa Kisiwani Rukuba na inatarajiwa kufunguliwa mwakani januari 2025
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo imesema maabara za Etaro sekondari ya somo la kemia na bailojia zimekamilika na zinafanya kazi.
Taarifa inasema maabara ya Fizikia inakamilishwa na ujenzi wake unachangiwa na Wanavijiji, mbunge wa jimbo na mfuko wa jimbo.
Chumba cha kompyuta kipo na kompyuta 25 tayari zimefungwa na wanafunzi wanazitumia kwaajili ya kujifunza.
Kompyuta hizo 25 zimenunuliwa na Northern Illinois University ya USA kama wadau wa elimu huku fedha za ufungaji wa miundombinu ya interne zimetolewa na chuo hicho huku kompyuta hizo na nyingine zitakazonunuliwa zitatumiwa na wanafunzi wa Kidato Cha Tano na sita
Aidha tenki la maji lenye ujazo wa lita 21,000 linajengwa shuleni hapo kwa ufadhili wa Northern Illnois University ya USA na ujenzi upo kwenye hatua za ukamilishwaji.
Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo kwa niaba ya wananchi ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa michango mingi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ya sayansi kwenye shule ndani ya jimbo.
Vilevile ameendelea kushukuru Northern Illinois University ya USA kwa ushirikiano wake wa kuboresha miundombinu ya elimu ya Etaro sekondari.
Mbunge huyo amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia miundombinu ya elimu ili kusaidia kuinua kiwango cha elimu.



Comments
Post a Comment