MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kudhihirisha ubora wake katika utoaji wa huduma baada ya kuibuka mshindi wa tuzo maalumu kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Tuzo hiyo ilitolewa Julai 3, 2026 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa mgeni rasmi katika maonesho hayo, huku mgeni wa heshima akiwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo. Kwa niaba ya TPA, tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Plasduce Mbossa.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dkt. George Fasha, alisema mafanikio hayo yanatokana na uongozi imara wa Bodi ya Wakurugenzi, ushirikiano wa wafanyakazi pamoja na dhamira ya taasisi hiyo ya kuendelea kuboresha huduma kwa wateja.
Amesema tuzo hiyo ni uthibitisho wa juhudi zinazoendelea kufanywa na TPA katika kuimarisha ufanisi wa huduma za bandari, kuongeza ubora wa utoaji wa huduma na kuendeleza mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya usafirishaji na biashara.
Dkt. Fasha ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, iliyowakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Ellinami Minja, kwa kutoa mwelekeo na usimamizi madhubuti ulioiwezesha mamlaka hiyo kuendelea kufanya vizuri na kupata heshima katika maonesho hayo ya kimataifa.
Aidha, amewapongeza wafanyakazi wote wa TPA kwa kujituma, kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia viwango vya ubora katika utoaji wa huduma, akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano na juhudi za pamoja.
"Napenda kuishukru Bodi ya Wakurugenzi na kuwapongeza wafanyakazi wote wa TPA kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa bidii na weledi. Tuzo hii ni ushahidi wa juhudi zetu za pamoja. Tusiridhike na mafanikio haya, bali tuongeze nguvu ili mwaka ujao tufanye vizuri zaidi," amesema Dkt. Fasha.
Amesisitiza kuwa TPA itaendelea kuboresha huduma zake, kutumia teknolojia za kisasa na kuimarisha uhusiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha bandari za Tanzania zinaendelea kuwa chaguo bora kwa biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ushindi huo unaongeza rekodi ya mafanikio ya TPA katika Maonesho ya Sabasaba na kuonyesha dhamira ya taasisi hiyo ya kuendelea kutoa huduma bora, zenye ufanisi na zinazokidhi matarajio ya wateja pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.



Comments
Post a Comment