Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kina mchango mkubwa katika kuandaa watumishi wenye weledi, maadili na uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Ridhiwani amesema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi mbalimbali, wakuu wa zamani wa chuo, wadau wa maendeleo na taasisi zilizoshirikiana na chuo hicho walishiriki katika hafla hiyo.
Amesema maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kutambua mchango wa watu binafsi na taasisi mbalimbali zilizosaidia kukijenga na kukiendeleza chuo hicho kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita. Katika hafla hiyo, vyeti na tuzo za shukrani zilitolewa kwa wahusika waliotoa mchango mkubwa katika mafanikio ya chuo.
Aidha,Mhe. Ridhiwani amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika mafunzo na maendeleo ya watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma serikalini.
Amesema Chuo cha Utumishi wa Umma kitaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga utumishi wa umma unaozingatia weledi, uwajibikaji na maadili, hatua ambayo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya Taifa.







Comments
Post a Comment