Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema utekelezaji wa kaulimbiu ya "Tunalipa Jana" umeendelea kuleta mafanikio makubwa, huku wastaafu wengi wakilipwa mafao yao kwa wakati mara tu baada ya kumaliza utumishi, mradi nyaraka zao zimekamilika na kuwasilishwa kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, amesema kaulimbiu hiyo, iliyoanzishwa Aprili mwaka huu, ni sehemu ya mkakati wa Mfuko wa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wanachama.
Amesema PSSSF imejipanga kuhakikisha mwanachama anayeanza safari ya utumishi anakuwa na taarifa sahihi na zinazohuishwa mara kwa mara ili kufikia kipindi cha kustaafu asiwe na changamoto yoyote ya kupata mafao yake.
"Dhamira yetu ni kuhakikisha mwanachama analipwa mafao yake siku ya kustaafu. Hiyo ndiyo tafsiri halisi ya kaulimbiu ya Tunalipa Jana. Tunataka kuondoa kabisa ucheleweshaji wa malipo kwa wanachama wanaokidhi vigezo," amesema Magambo.
Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2026/2027, Mfuko tayari umeanza kuchakata nyaraka za watumishi wanaokaribia kustaafu ili kuhakikisha mafao yao yanalipwa kwa wakati mara tu wanapostaafu.
Magambo amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarika kwa ukwasi wa PSSSF baada ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kulipa zaidi ya shilingi trilioni nne za deni la muda mrefu la michango ya wanachama.
Amesema hatua hiyo imeimarisha uwezo wa Mfuko kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, ikiwemo kulipa mafao kwa wakati na kuboresha huduma nyingine kwa wanachama.
Aidha, amebainisha kuwa PSSSF itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa, kuimarisha mifumo ya utunzaji wa taarifa za wanachama na kushirikiana kwa karibu na waajiri ili kuhakikisha kila mwanachama anayestahili anapata mafao yake kwa haraka, kwa usahihi na bila usumbufu.
Kwa upande wake, mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bi. Rosemary Makene, ameipongeza PSSSF kwa huduma bora baada ya kupokea mafao yake ya mkupuo mara tu baada ya tarehe yake ya kustaafu kufika.
Amesema aliwasilisha madai yake kwa njia ya mtandao na kufuatilia hatua zote za uchakataji hadi alipopokea malipo yake bila changamoto yoyote.
"Sikupata usumbufu wowote. PSSSF wanafanya kazi nzuri sana. Baada ya kustaafu, mwajiri anakamilisha jukumu lake, lakini PSSSF ndiyo mshirika wako wa karibu katika maisha ya ustaafu. Nawapongeza kwa huduma bora wanayoendelea kutoa," amesema Makene.
Kaulimbiu ya "Tunalipa Jana" ni sehemu ya mkakati wa PSSSF wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia, kuongeza ufanisi katika uchakataji wa mafao na kuhakikisha wanachama wote wanapata stahiki zao kwa wakati.






Comments
Post a Comment