Na Mwandishi Wetu, Misungwi
Jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuinua kiwango cha elimu zimeanza kuvuka mipaka ya Mkoa wa Mwanza, baada ya maafisa elimu kutoka halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Geita kutembelea wilaya hiyo kujifunza mbinu zilizoiwezesha kufanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa miaka mitatu mfululizo.
Ugeni huo ulifika Misungwi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza mikakati ya usimamizi wa elimu, ufuatiliaji wa taaluma na ushirikishwaji wa wadau, hatua zinazotajwa kuwa nguzo kuu za mafanikio ya halmashauri hiyo.
Akizungumza baada ya kikao cha kubadilishana uzoefu, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Jenoveva Chuchuba, alisema ujio wa maafisa hao ni ishara kwamba kazi inayofanywa na walimu, viongozi wa elimu na jamii imeanza kutambuliwa hata nje ya mkoa.
"Kwa miaka mitatu mfululizo tumekuwa tukifanya vizuri katika mitihani ya taifa. Hili limetokana na usimamizi wa karibu wa taaluma, ushirikiano wa walimu, viongozi na wazazi, pamoja na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kubaini changamoto na kuzitatua kwa wakati," alisema.
Alisema pamoja na juhudi za walimu, mchango wa wazazi umeendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio hayo, hususan kupitia mwitikio wao wa kuchangia chakula kwa wanafunzi shuleni.
Kwa mujibu wa Chuchuba, mpango huo umechangia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi, kuboresha umakini darasani na hatimaye kuongeza ufaulu katika mitihani ya taifa.
Baadhi ya maafisa elimu kutoka Mkoa wa Geita walisema walichagua kutembelea Misungwi baada ya kuvutiwa na mwenendo wake mzuri wa matokeo ya mitihani, wakiamini kuwa uzoefu huo utawasaidia kuboresha sekta ya elimu katika halmashauri zao.
Walisema wamejifunza mbinu mbalimbali za usimamizi wa shule, ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi, matumizi ya tathmini za kitaaluma na namna ya kuhamasisha ushiriki wa wazazi katika elimu ya watoto wao.
"Tunarejea Geita tukiwa na maarifa mapya. Tunatarajia kuyatumia kuboresha utendaji wetu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika halmashauri zetu," alisema mmoja wa maafisa hao.
Ziara hiyo inaakisi umuhimu wa halmashauri kujifunza kutoka kwa wenzao wenye mafanikio, huku ikionyesha kuwa kubadilishana uzoefu ni miongoni mwa njia zinazoweza kuharakisha maboresho ya sekta ya elimu nchini.











Comments
Post a Comment