MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe. Agnes Marwa, ameendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo kwa kuwasaidia kupata mikopo isiyo na riba ili kuwasaidia kukuza biashara zao na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Agnes amesema ameamua kujitoa kwa kutumia sehemu ya mshahara wake kugharamia riba ya mikopo hiyo, ili kuwaondolea changamoto ya kukosa dhamana inayowakwamisha wajasiriamali wengi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za kifedha na uwezeshaji wa moja kwa moja.
“Nimeamua kujinyima mimi na familia yangu ili kuhakikisha wajasiriamali hawa wanapata fursa ya kukua kiuchumi. Lengo langu ni kuona wanajenga biashara zao na kuboresha maisha yao,” amesema Mhe. Agnes
Baadhi ya wajasiriamali walionufaika na mpango huo wamesema msaada huo umewapa fursa ya kupata mitaji ambayo awali ilikuwa vigumu kuipata kutokana na kukosa dhamana.
Bibi Mango Chacha amesema bila msaada wa Mbunge Agnes asingepata nafasi ya kukopa, huku akieleza kuwa mkopo huo utamsaidia kupanua biashara yake.
“Kwa kweli kama si Mheshimiwa Agness Marwa nisingepata kabisa mkopo huu. Ninamshukuru sana kwa msaada huu,” amesema.
Naye Estar Adam amesema mafunzo ya ujasiriamali pamoja na dhamana waliyopewa yamewapa matumaini mapya ya kujikwamua kiuchumi na kuongeza kipato.
Kwa upande wake, mwakilishi wa CRDB Bank Foundation, Isaac Ibrahim, amesema taasisi hiyo imeingia ushirikiano na Mbunge Agness Marwa kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali wadogo kupata elimu ya fedha na fursa za mikopo.
Amesema mpango huo unalenga kuwafikia wananchi wanaokosa sifa za kukopesheka kutokana na changamoto ya dhamana, ili waweze kupata mitaji na kukuza biashara zao.
Mpango huo unaendelea kupongezwa na wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kuonekana kuwa suluhisho la changamoto ya mitaji kwa wajasiriamali wadogo.







Comments
Post a Comment