Balozi wa Amani Tanzania na Katibu wa Mahusiano wa Jumuiya ya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Mess Chengula, amepongeza hali ya amani na utulivu iliyoendelea kutawala jijini Mwanza, akisema ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa wananchi.
Akizungumza leo baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo, Chengula alisema ameridhishwa kuona shughuli za kijamii na kiuchumi zikiendelea, huku baadhi ya maduka yaliyokuwa yamefungwa yakifunguliwa tena na kuanza kutoa huduma.
"Ninawapongeza Watanzania kwa kuchagua amani siku hii ya leo. Furaha kubwa kwa binadamu ni kuona amani ikitawala mioyoni mwa watu," amesema.
Aidha, aliiomba Serikali kuendelea kusikiliza makundi mbalimbali yenye malalamiko ili kutatua changamoto kwa njia ya mazungumzo na kuimarisha utulivu nchini.
Chengula amesema amani huwezesha wananchi kujishughulisha kwa uhuru katika shughuli za uzalishaji mali, huku akisisitiza kuwa maridhiano yanayotarajiwa kufanywa kati ya Serikali, vyama vya siasa na makundi mbalimbali ya jamii ni hatua muhimu ya kuendeleza mshikamano wa Taifa.
Ameongeza kuwa ataendelea kuhamasisha utamaduni wa amani popote anapopata fursa, akieleza kuwa amani huanzia kwa kila mtu binafsi.


Comments
Post a Comment