Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

HISTORIA MPYA MAFINGA: SHULE YA SEKONDARI NDOLEZI YAANZA KUPOKEA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO

 

Na Mwandishi Wetu, Mafinga

SHULE ya Sekondari Ndolezi iliyopo Halmashauri ya Mji Mafinga, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, imeandika historia mpya baada ya kuanza rasmi kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano kwa mara ya kwanza. Hatua hii inatajwa kuwa ukombozi mkubwa utakaopanua fursa za elimu ya sekondari ya juu (A-Level) katika eneo hilo.

Akizungumza na wanafunzi wa kwanza waliowasili shuleni hapo, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Mwalimu Stephen Shemdoe, amesema lengo kuu la Halmashauri ni kuhakikisha wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini wanapata elimu bora itakayowezesha kupata matokeo mazuri na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Mwalimu Shemdoe amebainisha kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Kutokana na uwekezaji huo, amewataka wanafunzi kutumia fursa hiyo adhimu kusoma kwa bidii, kutunza mali za shule, na kuzingatia nidhamu ya hali ya juu.

"Matamanio ya Serikali ni kuona mnapata ufaulu mzuri kupitia malezi bora na elimu mnayopewa, ili muweze kutimiza ndoto zenu na kuwa rasilimali muhimu kwa Taifa," alisisitiza Mwalimu Shemdoe huku akiwaasa kujiepusha na tabia zinazoweza kuathiri masomo yao na badala yake kufuata sheria na taratibu za shule.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ndolezi, Mwalimu Hongera Swenya, amebainisha utayari wa shule hiyo katika kuwapokea wanafunzi hao wa kihistoria kwa mwaka wa masomo wa 2026, huku akieleza kuwa jumla ya wanafunzi 123 wamepangiwa kujiunga na shule hiyo.

Mwalimu Swenya aliongeza kuwa hadi kufikia jana Alhamisi, Julai 9, wanafunzi 16 walikuwa tayari wamesharipoti shuleni tayari kuanza masomo. Shule hiyo inatoa michepuo ya Sayansi ambayo ni PCB (Fizikia, Kemia, Baiolojia), PCM (Fizikia, Kemia, Hisabati), na PGM (Fizikia, Jiografia, Hisabati), huku zoezi la mapokezi likiendelea vyema.





Comments