TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO MZITO WA COP12, NCHI 10 KUKUTANA DAR ES SALAAM KUJADILI UCHUMI WA BULUU
Na MASHAKA MHANDO, Tanga
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) utakaofanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 9 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari leo jijini Tanga, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa ustawi wa mazingira na uchumi wa taifa.
Naibu Waziri huyo alizitaja nchi zitakazoshiriki kwenye mkutano huo kuwa ni pamoja na wenyeji Tanzania, Kenya, Somalia, Afrika Kusini, Msumbiji, Ufaransa, Comoro, Ushelisheli (Seychelles), Mauritius na Madagascar.
Alifafanua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi ambao unahusu uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa mazingira ya bahari kwenye maeneo ya Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi. Kwa mujibu wa Naibu Waziri Kwagilwa, mkataba huo ulisainiwa Juni 21, 1985, na unatekelezwa chini ya usimamizi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
Alisema kupitia mkataba huo, nchi wanachama hukutana kila baada ya miaka miwili kujadili utekelezaji wa shughuli, mipango, pamoja na mikakati ya mkataba.
"Mkutano wa COP12 utajadili utekelezaji wa mpango mkakati wa mkataba kwa miaka miwili, kupokea taarifa za mapato na matumizi, pamoja na kujadili suala la urejeshwaji wa mifumo ya ikolojia na hifadhi za baharini," alisema Mhe. Kwagilwa na kuongeza:
"Majadiliano yatafanyika juu ya namna ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira kwa kudhibiti taka za plastiki na mafuta yanayomwagika baharini ambayo yanaleta athari kubwa kimazingira."
Mhe. Kwagilwa aliongeza kuwa kutakuwa pia na majadiliano kuhusu utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa ya Bioanuai za bahari zilizo nje ya mamlaka za kitaifa (BBNJ). Mkutano huo unatarajiwa kupitisha mikakati ya kuimarisha Uchumi wa Buluu ulio endelevu na stahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kaulimbiu ya kitaifa ya mwaka huu inasema: "Kuelekea Uchumi wa Buluu Endelevu katika Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi kwa Manufaa ya Watu na Mazingira Asili: Safari ya Miaka 40."
Katika taarifa yake, Naibu Waziri Kwagilwa alianza kwa kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri wenye maono makubwa katika kuipa kipaumbele sekta ya mazingira na uhifadhi wa rasilimali za bahari. Mbali na hayo, alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatambua Sekta ya Uchumi wa Buluu kuwa miongoni mwa sekta za kimkakati za kuleta mageuzi ya maendeleo endelevu yanayochangia ukuaji wa kiuchumi na kijamii.
"Uchumi wa Buluu unahusisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii. Kutokana na Tanzania kuwa nchi ya pwani, ina fursa kubwa ya kunufaika kupitia nishati, usafirishaji, viwanda, utalii na mazingira," alisisitiza.
Awali, kabla ya Naibu Waziri kuzungumza, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian alisema Mkoa huo umeanza kufanya tafiti na stadi kuhusu namna unavyoathirika na mabadiliko ya tabianchi.
Mkuu huyo wa mkoa alisema maeneo ambayo wameanza kuyafanyia kazi ni Sekta ya Uvuvi na Kilimo, ambapo kwenye uvuvi imegundulika kuwa uwezo wa wavuvi kuvua umepungua kwa asilimia 50 kutokana na sababu kadhaa zinazohusiana na mabadiliko hayo.






Comments
Post a Comment