Naibu Waziri wa Ofisi ya waziri Mkuu TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, amesema Serikali itafanya tathmini ya kina kuhusu mahitaji ya ujenzi wa shule za sekondari katika vijiji vya Isaba (Buruma), Magunga (Mirwa) na Nyamsangura (Bwiregi), kufuatia ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Butiama, Dkt. Charles Mahera.
Dkt. Mahera ameibua hoja hiyo bungeni akieleza kuwa wananchi wa vijiji hivyo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa shule za sekondari, hali inayowalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu.
Dkt. Mahera alitaka kujua ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule katika maeneo hayo ili kuboresha upatikanaji wa elimu kwa watoto.
Akijibu swali hilo, Dkt. Dugange amesema kuwa kwa mujibu wa sera na miongozo ya Serikali kuhusu elimu ya sekondari, ujenzi wa shule mpya huzingatia mahitaji ya kila kata.
Ameeleza kuwa pale ambapo kata ina idadi kubwa ya wanafunzi au mazingira yanayoonyesha uhitaji wa shule nyingine, Serikali inaweza kuidhinisha ujenzi wa shule mpya ndani ya kata hiyo.
Ameongeza kuwa Serikali imepokea rasmi ombi la Mbunge huyo na itafanya tathmini katika vijiji vilivyotajwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo umbali wanaotembea wanafunzi kufikia shule za sekondari zilizopo pamoja na idadi ya wanafunzi wanaohitaji huduma hiyo.
Dkt. Dugange amesema endapo tathmini hiyo itabaini kuwa maeneo hayo yanakidhi vigezo vilivyowekwa, Serikali itayajumuisha katika mipango yake ya maendeleo na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo, hatua inayolenga kusogeza huduma za elimu karibu zaidi na wananchi na kuongeza fursa kwa watoto kupata elimu ya sekondari.

Comments
Post a Comment