Na Dawati la Habari Polisi; Mwanza.
Mtu mmoja amefariki dunia huku wengine saba wakijeruhiwa kufuatia mlipuko wa baruti uliotokea leo Julai 1, 2026, majira ya saa 12:46 asubuhi katika kibanda cha kahawa kilichopo Mtaa wa Sahwa ya Juu, Kata ya Lwanhima, Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amesema aliyefariki ni Marco Msenyere (52), mpasua mawe na mkazi wa Semba-Lwanhima. Amesema marehemu alikuwa amefika katika kibanda hicho kunywa kahawa akiwa na begi dogo lililokuwa na baruti.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mlipuko huo ulisababishwa na uzembe wa utunzaji wa baruti, baada ya marehemu kuweka begi lenye baruti karibu na jiko la mkaa lililokuwa linawaka. Joto kutoka kwenye jiko hilo lilisababisha baruti kulipuka.
Majeruhi wa tukio hilo ni Daudi Joseph Baraka (54), Emmanuel Luhangwa Joseph (40), Yusufu Rajabu Nasoro (20), Zawadi Saimon Ndukeji (27), James Hussein Ntugo (33), Joseph Muyagingwa Englibert (22), na Marco Mahunge Chandanoba (45). Wote wamepatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana (Butimba), huku mmoja akihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa matibabu zaidi.
Kamanda Mutafungwa amesema eneo la tukio limekaguliwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Tume ya Madini Mkoa wa Mwanza, na kubainika kuwa sasa ni salama kwa matumizi ya wananchi.
Ametoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaomiliki au kutumia baruti bila vibali halali ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Kwa upande wake, Afisa wa Tume ya Madini Mkoa wa Mwanza, Deus Makuli, amesema ni kosa kisheria kumiliki au kutumia baruti bila leseni, akibainisha kuwa marehemu hakuwa na kibali cha kumiliki vilipuzi hivyo. Pia amewataka viongozi wa mitaa kuhakikisha shughuli zote za ulipuaji wa mawe zinafanyika kwa kufuata sheria na taratibu.
Baadhi ya wakazi wa Lwanhima wameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kuahidi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaotumia vilipuzi kinyume cha sheria, ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia.










Comments
Post a Comment