Na MASHAKA MHANDO, Korogwe
SERIKALI imempa mwezi mmoja hadi Julai 31 mwaka huu mkandarasi anayekarabati Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Hale wilayani Korogwe mkoani Tanga, kukamilisha mradi huo wa Shilingi Bilioni 64 (Dola Milioni 24.81) ambao kwa sasa umefikia asilimia 83 ya utekelezaji nyanjani.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akikagua maendeleo ya kituo hicho jana, Juni 29, 2026, ambapo alisisitiza kuwa Serikali haitakuwa tayari kuongeza muda wa mkataba hata kwa siku moja ili wananchi wapate nishati ya uhakika.
"Mkandarasi ahakikishe anakamilisha mradi huu kwa muda uliopangwa ifikapo Julai 31 mwaka huu, ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika, sambamba na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi," alisema Waziri Ndejembi.
Akifafanua umuhimu wa mradi huo, Waziri Ndejembi alibainisha kuwa kukamilika kwa ukarabati wa kituo hicho kutaimarisha ufanisi wa uzalishaji wa umeme, kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo kwa uhakika, na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi katika Mkoa wa Tanga na maeneo ya jirani.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji Umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Timoth Mgaya, aliungana na maelekezo hayo na kufafanua zaidi kuhusu ukubwa wa uwekezaji huo unaogharimu takribani Shilingi Bilioni 64.
Mhandisi Mgaya alithibitisha kuwa kazi za ukarabati zinaendelea kwa kasi kama ilivyopangwa, huku zikiwa zimebakiza hatua chache kufikia kilele chake kabla ya hatua ya mwisho ya makabidhiano rasmi.




Comments
Post a Comment