▪️Waziri Mavunde akutana na Mwekezaji wa Kiwanda cha Kuzalisha Goroli za Chuma
▪️Ni kiwanda cha Oriental Casting and Forging Ltd cha China
▪️Kiwanda kikubwa kujengwa Buzwagi Kahama
▪️Tanzania yajipanga kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa za migodini Afrika
📍 Dar es salaam
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde leo Juni 30, 2026 amekutana na Mkurugenzi Mkuu na Mmiliki wa Kiwanda cha Kuzalisha Goroli za Chuma “Steel balls” Bw. Hou Songcun kujadiliana juu ya uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini ili kuzalisha bidhaa za migodini.
Waziri Mavunde amewakaribisha wawekezaji wao kwenye eneo lililotengwa na serikali la Buzwagi Special Economic Zone lililopo wilayani Kahama,Shinyanga kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuzalisha bidhaa za migodini ili kuwahudumia wachimbaji wakubwa na wadogo nchini.
Waziri Mavunde amesema serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu imejipanga kuhakikisha inavutia uwekezaji mkubwa kwenye uzalishaji wa bidhaa za migodini ili Tanzania kuwa kitovu za usambazaji wa bidhaa hiyo barani Afrika.
“Lengo letu ni kuona wachimbaji wakubwa na wadogo hapa nchini wanapata bidhaa nyingi za kuzalisha madini pasipo kutegemea uagizwaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi," amesema Mavunde.
Naye, Mmiliki na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oriental Casting and Forging Ltd Bw. Hou Songcun amesema Kampuni yake ipo tayari kufanya uwekezaji mkubwa wa bidhaa za migodini nchini kwa kuwa Tanzania ni nchi ambayo ina mazingira mazuri ya uwekezaji na kwamba sekta ya madini inakua kwa kasi kubwa sana hivyo ni sehemu salama na rafiki ya kufanya uwekezaji ambao utakuwa suluhisho la upatikanaji wa bidhaa za migodini kwa urahisi zaidi.









Comments
Post a Comment