RAIS DKT. MWINYI AISHUKURU INDIA KWA KUIMARISHA USHIRIKIANO, APOKEA MWALIKO RASMI WA KUTEMBELEA INDIA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya India kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na Zanzibar katika sekta mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 30 Juni 2026, alipokutana na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bishwadip Dey, pamoja na ujumbe wake, waliofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza uwekezaji unaofanywa na wawekezaji na taasisi binafsi za India nchini na kueleza utayari wa Zanzibar kuimarisha ushirikiano na India katika elimu ya ufundi na mafunzo ya amali.
Aidha, amesifu mchango wa Taasisi ya Teknolojia ya India Madras, IIT Madras Zanzibar, katika utoaji wa elimu na mafunzo ya kitaalamu, pamoja na kuleta mageuzi katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. IIT Madras Zanzibar ni kampasi ya kwanza ya kimataifa ya taasisi hiyo nje ya India.
Kwa upande wake, Balozi Bishwadip Dey amemkabidhi Rais Dkt. Mwinyi mwaliko rasmi kutoka kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya India, Mhe. C. P. Radhakrishnan, wa kutembelea India mwezi Julai 2026. Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi pia anatarajiwa kutembelea makao makuu ya IIT Madras yaliyopo Chennai.
Vilevile, Balozi Dey ameihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa India itaendelea kuimarisha ushirikiano na Zanzibar katika sekta mbalimbali za maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.












Comments
Post a Comment