INADES-FORMATION TANZANIA YASHIRIKIANA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS KUANDAA MPANGO WA MAZINGIRA WILAYA YA BAHI
By Prosper Makene
Katika juhudi za kuhakikisha Tanzania inafikia azma ya kuwa nchi ya kijani ifikapo mwaka 2050, Shirika la INADES-Formation Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais – Idara ya Mazingira limeandaa kikao kazi cha kuandaa Mpango wa Usimamizi wa Mazingira wa Wilaya ya Bahi, kwa kushirikisha wataalamu kutoka Wilaya za Chemba na Kondoa.
Akifungua kikao hicho Leo katika ofisi ya Makamu wa Rais, Mtumba mjini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais – Idara ya Mazingira, Dk. Paul Deogratius, alisema ushiriki wa Wilaya za Chemba na Kondoa utasaidia kubadilishana uzoefu katika mchakato wa kuandaa mpango huo kwa Wilaya ya Bahi.
Alieleza kuwa mipango ya usimamizi wa mazingira katika ngazi ya wilaya ni takwa la kisheria na ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za mazingira zinazozikabili halmashauri nchini.
"Kitaifa, zimetambuliwa zaidi ya changamoto 13 za mazingira, huku kila wilaya ikiwa na changamoto zake kulingana na mazingira na shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika eneo husika. Hivyo, uwepo wa mpango wa usimamizi wa mazingira ni muhimu katika kutoa mwongozo wa namna ya kuzikabili changamoto hizo," alisema Dk. Deogratius.
Aliongeza kuwa maandalizi ya mpango huo yataisaidia Tanzania kutekeleza mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kufikia lengo la kuwa nchi ya kijani ifikapo mwaka 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa INADES-Formation Tanzania, Bi. Jacqueline Nicodemus, alisema ushirikiano na Ofisi ya Makamu wa Rais – Idara ya Mazingira ni muhimu ili kuhakikisha mipango hiyo inaandaliwa kwa kuzingatia miongozo, sera na mikakati ya kitaifa ya usimamizi na uhifadhi wa mazingira.
Aidha, aliomba Ofisi hiyo kushiriki katika uzinduzi wa mipango ya usimamizi wa mazingira ya Wilaya za Chemba na Kondoa, akisema ushiriki huo utatoa msukumo na kuhamasisha wadau mbalimbali kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya nchi.
Nao washiriki wa kikao hicho walisisitiza kuwa mipango ya usimamizi wa mazingira katika wilaya hizo inapaswa kuendana na vipaumbele vya kitaifa, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, mipango kabambe ya maendeleo, Sera ya Taifa ya Mazingira pamoja na miongozo mingine ya uhifadhi wa mazingira.
Vilevile, walieleza umuhimu wa kupata mwongozo wa kitaalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais – Idara ya Mazingira katika hatua za kuandaa na kupitia rasimu ya Mpango wa Usimamizi wa Mazingira wa Wilaya ya Bahi, ili kuhakikisha unakidhi viwango na matakwa ya kitaifa.

Comments
Post a Comment