CRDB Bank imeendelea kuthibitisha kuwa rasilimali muhimu zaidi katika mafanikio ya taasisi ni watu wake, kwa kuendesha programu ya Wellness Day inayolenga kuimarisha afya ya mwili, akili na ustawi wa wafanyakazi, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kujenga nguvu kazi yenye tija, ubunifu na ufanisi.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa programu hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Edward Mpina, amesema benki hiyo inaamini kuwa mafanikio ya biashara hayawezi kutenganishwa na afya ya wafanyakazi wake, ndiyo maana imeendelea kuwekeza katika mipango inayowalinda na kuwajengea mazingira bora ya kufanya kazi.
Mpina amesema dhana ya wellness ni pana zaidi kuliko kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, kwani inajumuisha afya ya akili, ustawi wa kihisia, uwezo wa kukabiliana na changamoto za kazi na maisha pamoja na kujenga usawa kati ya kazi na familia.
Ameeleza kuwa katika mazingira ya kisasa ya kazi, wafanyakazi hukabiliwa na shinikizo la kufikia malengo ya biashara, kutimiza viashiria vya utendaji (KPIs), kutoa huduma bora kwa wateja na kukamilisha majukumu kwa wakati, hali ambayo inaweza kuathiri afya ya akili endapo haitasimamiwa vizuri.
"Hatutaki mafanikio ya CRDB yaje kwa gharama ya afya ya wafanyakazi wetu. Tunataka kila mfanyakazi awe na afya njema ya mwili na akili ili afanye maamuzi sahihi, awe mbunifu, atoe huduma bora kwa wateja na achangie ukuaji endelevu wa benki," amesema Mpina.
Amesema kupitia programu hiyo, benki inawapa wafanyakazi fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa afya, kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya pamoja na elimu kuhusu lishe bora, mazoezi, afya ya akili na mbinu za kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Aidha, amesema mpango huo hauwalengi wafanyakazi pekee, bali pia familia zao, akieleza kuwa familia yenye afya na utulivu hujenga mfanyakazi mwenye ari, utulivu wa akili na uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa CRDB, Idara ya Rasilimali Watu imekuwa ikishirikiana na wataalamu wa afya kuhakikisha elimu na huduma za ustawi zinawafikia wafanyakazi katika kanda zote za benki, ikiwa ni sehemu ya kujenga utamaduni wa kuthamini afya mahali pa kazi.
Mbali na kuendelea kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika sekta ya fedha kwa ubunifu wa huduma na teknolojia, CRDB imejipambanua pia kwa kuwekeza katika ustawi wa wafanyakazi wake, ikiamini kuwa afya bora ndiyo msingi wa huduma bora kwa wateja na mafanikio endelevu ya taasisi.
Programu ya Wellness Day hufanyika kwa mfumo wa kanda, na safari hii imefanyika jijini Dodoma, ikiwakutanisha wafanyakazi wa benki hiyo katika shughuli mbalimbali za uchunguzi wa afya, ushauri wa kitaalamu na elimu kuhusu namna ya kuishi maisha yenye afya na kuongeza tija kazini.





Comments
Post a Comment