📍Wafanyabiashara wakiri kumalizika kwa uhasama wa 'Paka na Chui', taasisi za fedha zaahidi ushirikiano
NA Mashaka Mhando, Tanga
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, ambapo makusanyo ya kodi yamepanda kutoka Shilingi Bilioni 531 mwaka 1996/1997 hadi kufikia Shilingi Trilioni 32 kwa mwaka uliopita.
Hayo yamebainishwa leo wakati wa matembezi maalum ya hisani na mazoezi yaliyoanzia katika ofisi za TRA Mkoa wa Tanga hadi viwanja vya Usagara, yakiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya mamlaka hiyo na maandalizi ya Tuzo ya Rais kwa Mlipakodi Bora.
Akizungumza baada ya kuongoza matembezi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, aliipongeza TRA kwa hatua kubwa iliyopigwa na kueleza kuwa Mkoa wa Tanga umefanya vizuri kwa kuvuka malengo ya makusanyo kwa asilimia 100.
Balozi Batilda alieleza kuwa kukua kwa shughuli za Bandari ya Tanga, mipaka ya Horohoro, na wilayani kumeufanya mkoa huo kuipiku Arusha na kushika nafasi ya sita kitaifa katika ukusanyaji wa mapato.
"Kila sekta iainishwe katika ukusanyaji wa mapato. Tanga ina fursa nyingi, tunapaswa kuelekeza nguvu zaidi ili tushike nafasi ya pili kitaifa. Pia nawapongeza kwa kusogeza huduma kwa kufungua ofisi mpya Mkata (Handeni) na Kipumbwi (Pangani). Watu waache magendo na walipe ushuru, hakuna sababu ya kukwepa," aliagiza Balozi Dkt. Batilda.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa falsafa yake ya kukusanya kodi bila kutumia nguvu na mabavu, jambo ambalo limeleta tija kubwa nchini.
*Historia na Mapinduzi ya Kidijitali*
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, CPA Castro John, alikumbusha kuwa mamlaka hiyo ilianzishwa mwaka 1996 na Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa, kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwazi.
CPA Castro alibainisha kuwa siri kubwa ya ukuaji wa makusanyo ni kuhama kutoka kwenye mifumo ya zamani ya mikono (*manual*) na kwenda kwenye mifumo ya kiteknolojia, sambamba na kuongezeka kwa mwamko wa ulipaji kodi kwa hiari.
Aliongeza kuwa katika kuelekea miaka 30 ijayo, chini ya kaulimbiu isemayo *'Kulipa Kodi ni Uzalendo na Ushujaa, Lipa Kodi kwa Maendeleo Yetu'*, TRA inalenga kuboresha zaidi mifumo na kuongeza wigo wa wafanyabiashara, huku akibainisha kuwa Rais ameridhia ajira mpya za watumishi zaidi ya 2,000 kuongeza nguvu kazi.
*Kauli za Wafanyabiashara na Taasisi za Fedha*
Akitoa salamu za wafanyabiashara, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga, Fredy Mmasy, alipongeza mamlaka hiyo na kufichua kuwa Mkoa wa Tanga ulikuwa na lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 425, lakini hadi sasa wamefanikiwa kukusanya Bilioni 495 hatua inayotokana ushirikiano uliopo baina ya TRA na walipa kodi.
"Zamani uhusiano wa wafanyabiashara na TRA ulikuwa kama Paka na Chui, lakini sasa tupo pamoja. TRA mmekua, sasa nendeni mkakijaze kibubu kwa kuongeza wafanyabiashara zaidi," alisema Mmasy.
Nao mameneja wa taasisi za kifedha, Hajra Mmambe kutoka Benki ya Azania na Dkt. Mussa Kamendu kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), waliahidi kuendeleza ushirikiano thabiti ili kuhakikisha kodi inakusanywa kwa usahihi na bila vikwazo.
Mwisho, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba, alihitimisha kwa kuwapongeza washiriki wa matembezi hayo na kueleza jinsi TRA ilivyoshirikiana na wilaya hiyo kusaidia usajili wa vikundi 202 vya wajasiriamali ili viweze kukopesheka na kurasimisha biashara zao.





Comments
Post a Comment