Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amesema kuwa historia ya Tanzania katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika itaendelea kubaki alama isiyofutika, akisisitiza kuwa baada ya ushindi wa ukombozi wa kisiasa, mataifa ya Afrika yanapaswa kuelekeza nguvu zake katika kujikomboa kiuchumi kupitia mshikamano, ushirikiano na maendeleo ya pamoja.
Akizungumza leo Jun 21,2026 wilayani Kongwa Mkoani Dodoma alipotembelea Makaburi na Kambi ya Kihistoria ya wapigania uhuru wa Chama cha SWAPO wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah amesema Tanzania iliandika historia ya kipekee kwa kuwafungulia milango wapigania uhuru, kuwapatia ardhi ya kuishi na kufanya mafunzo, pamoja na kuwalinda hadi walipofanikisha ukombozi wa Namibia na mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika.
Amesema wananchi wa Namibia wataendelea kuikumbuka Tanzania kwa mchango wake mkubwa, akibainisha kuwa uhusiano wa nchi hizo mbili haujajengwa kwa misingi ya diplomasia pekee, bali umejengwa kwa historia ya pamoja, mshikamano na damu ya mashujaa waliopigania uhuru wa Afrika.
"Tunabeba deni kubwa la shukrani kwa Tanzania. Mchango wenu hauwezi kufutika katika historia ya Namibia. Leo tunapaswa kulinda urithi huo kwa kufanya kazi pamoja na kuhakikisha tunazikomboa nchi zetu na Bara letu kiuchumi," amesema.
Rais huyo amesisitiza kuwa kizazi cha sasa kina wajibu wa kutafsiri mafanikio ya ukombozi wa kisiasa kuwa maendeleo ya kiuchumi kwa kuimarisha biashara, uwekezaji, viwanda, elimu, teknolojia na ushirikiano wa kikanda ili wananchi wanufaike na uhuru uliopatikana kwa gharama kubwa.
Akiwa katika eneo hilo la kihistoria, alipokea pia maombi kutoka kwa baadhi ya familia zilizotengana wakati wa harakati za ukombozi, ambapo baadhi ya watoto walibaki Tanzania huku wazazi wao wakirejea Namibia baada ya uhuru. Kutokana na hali hiyo, aliahidi kuwa Serikali ya Namibia itashirikiana na Serikali ya Tanzania kuwatafuta watoto hao na kuwaunganisha na familia zao, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuhifadhi historia na kurejesha utu wa familia zilizoathiriwa na mapambano ya ukombozi.
Aidha, amesema Kongwa itaendelea kuwa kumbukumbu muhimu ya historia ya ukombozi wa Afrika, kutokana na mchango wake wa kuwahifadhi na kuwalea wapigania uhuru kutoka mataifa mbalimbali, huku akitoa wito wa kuendelea kuenzi maeneo hayo ili vizazi vijavyo vijifunze thamani ya mshikamano wa Waafrika.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah alitembelea kiwanja cha Ubalozi wa Namibia kilichopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, ambako alipokelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi.
Akiwa katika ziara hiyo, alipata maelezo kuhusu Mpango Kabambe wa Mji wa Serikali na maendeleo ya utekelezaji wake kutoka kwa viongozi na wataalamu wanaousimamia mradi huo.
Kama ishara ya kuendeleza urafiki, mshikamano na uhusiano wa kidiplomasia uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya Tanzania na Namibia, Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah alipanda mti katika kiwanja cha Ubalozi wa Namibia na kuupa jina la "UMOJA TREE", akieleza kuwa mti huo utaendelea kuwa alama ya umoja, urithi wa pamoja na dhamira ya mataifa hayo mawili kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.







Comments
Post a Comment