Kutoka: Dawati la Habari Polisi Mwanza
Katika mwendelezo wa ukaguzi wa magari ya shule hususan katika kipindi hiki cha likizo, Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limeendelea na zoezi la ukaguzi likiwa na lengo la kuboresha huduma ya usafiri na kuimarisha usalama wa wanafunzi.Zoezi hilo lililozinduliwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Dcp Wilbrod Mutafungwa tarehe 18.06.2026 limeendelea leo, Juni 26, 2026, katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyang’homango iliyopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, ambapo jumla ya magari 25 yamekaguliwa.
Akizungumza na madereva pamoja na walezi wa wanafunzi wakiwemo ma-patron na ma-matron, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Misungwi, ASP Maris Isomba, amesema kuwa lengo kuu la ukaguzi huo ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama wanapokwenda na kurudi kutoka shuleni.
Aidha, ASP Isomba amekemea tabia ya baadhi ya wamiliki wa magari ya shule kuweka vioo vya giza (tinted). Amesema kitendo hicho ni kinyume cha sheria kwa magari ya usafiri wa umma na yanayobeba wanafunzi kwani kinaweza kuchochea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
"Magari ya shule yanatakiwa kuwa na vioo angavu ili kuruhusu mtu yeyote kuona mazingira ya ndani na kuhakikisha watoto wako salama," alisisitiza ASP Isomba.
Pia ametoa wito kwa wamiliki ambao bado hawajapeleka magari yao yakakaguliwe kuhakikisha wanatimiza takwa hilo la kisheria ambapo amewaonya watakaokaidi na kwamba watafuatwa kwenye shule zao na magari yatakayobainika kuwa mabovu yatapigwa marufuku kutoa huduma hadi yarekebishwe na kukaguliwa tena.
Naye Sajenti Juliana Nyambuka, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Misungwi, amewataka madereva na walezi hao kuwalinda watoto na kuzuia vitendo vya ukatili wawapo kwenye vyombo vya usafiri.
"Ukatili wa kijinsia ni sawa na mauaji mtoto akishalawitiwa, maisha yake yote yanakuwa yameharibiwa," alisema Sajenti Juliana.
Kwa upande wao, madereva na wasimamizi wa magari hayo wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi hilo muhimu. Wameahidi kuzingatia elimu waliyopewa, kufuata sheria na taratibu za usalama barabarani pamoja na kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.
"Ukaguzi huu unatukumbusha kutekeleza wajibu wetu na kubaini mapungufu yaliyopo kwenye magari yetu. Ni jambo zuri na tutalifanyia kazi." alisema Paschal Charles, Dereva.
"Kwa kweli nimepata elimu nzuri ya kuwa makini na kuwalinda watoto wasifanyiwe ukatili wa kijinsia. Nawaomba madereva wenzetu wazingatie sheria ili kulinda watoto na watumiaji wengine wa barabara." alisema Matron Cothorata
"Elimu hii itatusaidia sana katika matengenezo na urekebishaji wa magari yetu. Tunashukuru sana kwa juhudi hizi za askari wetu wa Misungwi." alisema Sadiki Damasi, Dereva









Comments
Post a Comment