WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kulinda amani, usalama wa wananchi na rasilimali za Taifa na haitamvumilia mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa nchi.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Juni 27, 2026) alipowasalimia wananchi wa Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kufuatilia taarifa kuhusu watu wanaodaiwa kupanga au kufadhili vitendo vinavyoweza kuvuruga amani ya nchi na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
"Hatutafanya mzaha na mtu wa aina hiyo. Tumepewa jukumu la kuilinda nchi yetu na watu wake, na hatutafanya mchezo kwenye jambo hilo."
Amesema Serikali haina mgogoro na chama chochote cha siasa kwa kuwa vyama hivyo vinatambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda amani, usalama wa Taifa na wananchi wake wakati wote.
"Hatuna ugomvi na chama chochote cha siasa. Lakini tuna jambo ambalo ni kipaumbele, usalama wa Tanzania na usalama wa Watanzania."
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji bila hofu.
Pia amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Singida ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa barabara, reli ya kisasa (SGR), uwanja wa ndege pamoja na miradi ya maji, afya na elimu kwa lengo la kuboresha huduma za wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Singida kuhakikisha fedha za maendeleo zinaelekezwa katika utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi, huku mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ikiendelea kuwafikia walengwa kwa wakati.






Comments
Post a Comment