WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu ya juu kwa kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ili kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Juni 27, 2026) alipoweka jiwe la msingi la Jengo la Taaluma la Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Singida.
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa jengo hilo unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha mazingira ya elimu ya juu na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
"Leo hii jengo hili la chuo chetu liko Singida. Hii ni hatua kubwa sana. Hongereni bodi, hongereni chuo, hongereni wanafunzi. Tunawatakia kila la heri," amesema.
Aidha, amewapongeza wahandisi, washauri na wakandarasi wazawa wanaotekeleza mradi huo akisema ushiriki wao unaonesha uwezo wa Watanzania katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
"Nimefurahishwa kwamba wahandisi wanaojenga ni wazawa, kwa sababu pia Mheshimiwa Rais alielekeza kwamba lazima tujenge uchumi unaomilikiwa na Watanzania na kujenga sekta binafsi ya ndani sambamba na uwekezaji kutoka nje," amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kuwekeza katika vyuo vya elimu ya juu ili kuongeza upatikanaji wa elimu bora, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuimarisha tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia pamoja na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa.
Amesema Wizara ya Fedha itaendelea kuhakikisha rasilimali za Serikali zinaelekezwa katika miradi yenye tija kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Pallangyo, amesema jengo hilo la taaluma lina ukubwa wa mita za mraba 9,250 na litakuwa na kumbi za mafunzo, madarasa, kumbi za mihadhara, ukumbi wa mikutano pamoja na ofisi za watumishi.
Amesema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 13.5 umefikia asilimia 63 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2026. Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa mabweni ili kukidhi ongezeko la wanafunzi litakalotokana na kukamilika kwa mradi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Prof. Jehovaness Aikaeli, amesema bodi itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati, huku akieleza kuwa mradi huo utachangia kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi kwa maendeleo ya Mkoa wa Singida na Taifa kwa ujumla.
Naye, Mhandisi Mkazi Mshauri wa Mradi, Henry Chundu, amesema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi wapatao 3,500 kwa wakati mmoja na limejengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa, ikiwemo mifumo ya usalama dhidi ya moto, matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na miundombinu ya kuvuna maji ya mvua.








Comments
Post a Comment