Na Mwandishi Wetu
UJUMBE kutoka Wizara ya Afya ya Namibia pamoja na wafanyabiashara walioambatana na Rais wa Namibia katika ziara yake ya hivi karibuni umetembelea Hospitali ya Kairuki na kujionea maendeleo ya huduma za afya, elimu ya tiba na uzalishaji wa dawa zinazotolewa na taasisi hiyo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kairuki, Dk, Sia Kiwia, alisema wageni hao walipata fursa ya kutembelea idara mbalimbali na kujifunza teknolojia za kisasa zinazotumika katika utoaji wa huduma za afya nchini Tanzania.
Alisema moja ya maeneo yaliyowavutia zaidi ni huduma ya matibabu kwa kutumia teknolojia ya HIFU (High-Intensity Focused Ultrasound), mtambo unaowezesha kuondoa uvimbe bila kufanyika upasuaji.
“Wameweza kuona mtambo wetu wa HIFU unaotibu uvimbe mbalimbali kwenye matiti, ini, kongosho, kizazi na tezi dume kwa wanaume Pia wamejionea aina za wagonjwa wanaoweza kufaidika na teknolojia hii na mchango wake katika kuboresha huduma za afya,” alisema Kiwia.
Aidha, alisema ujumbe huo ulifahamishwa kuhusu kituo cha Kairuki Green IVF kinachotoa huduma za uzazi kwa njia ya upandikizaji wa viinitete (IVF), ambapo ulijifunza kuhusu huduma zinazotolewa na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, kituo hicho tayari kimefanikiwa kupata zaidi ya watoto 150 waliozaliwa hai kupitia huduma za IVF, huku baadhi yao wakiwa tayari wameanza masomo ya awali.
Alisema kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali ikiwemo ushauri wa kitabibu ana kwa ana na kwa njia ya mtandao, vipimo, ushauri nasaha, pamoja na uhifadhi wa mbegu za kiume, mayai ya wanawake na viinitete.
“Karibuni tumezindua mtambo wa kisasa wa kusaidia upevushaji wa mayai na kuongeza uwezekano wa viinitete kupandikizwa kwa mafanikio,Teknolojia hiyo pia ina uwezo wa kufanya uchunguzi wa vinasaba ili kubaini changamoto zinazoweza kusababisha mimba kuharibika kabla ya kupandikiza kiinitete,” alisema Kiwia
Mbali na huduma za afya, wageni hao walipata fursa ya kujifunza kuhusu mchango wa Kairuki katika elimu ya tiba kupitia Chuo cha Kairuki, ambapo baadhi ya madaktari waliokuwa kwenye ujumbe huo waliwahi kupata mafunzo na kuhitimu katika taasisi hiyo.
Dkt. Kiwia alisema wageni hao walionesha nia ya kuendeleza ushirikiano na Tanzania ili kuboresha sekta ya afya nchini mwao kupitia kubadilishana uzoefu na mafunzo ya kitaalamu
Vilevile, alisema walielezwa kuhusu Kiwanda cha Dawa cha Kairuki Pharmaceutical Industries kilichopo Kibaha, kinachozalisha dawa mbalimbali ikiwemo antibiotiki pamoja na kemikali maalumu zinazotumika katika matibabu ya wagonjwa wenye matatizo ya figo.
Alisema ziara hiyo imeonesha kiwango cha maendeleo ya sekta ya afya nchini na uwezo wa taasisi za ndani kutoa huduma za kisasa zinazoweza kuvutia wagonjwa na wataalamu kutoka mataifa mengine ya Afrika.






Comments
Post a Comment