Waziri wa Ulinzi na jeshi la kujenga Taifa (JKT)Dkt Rhimo Nyansaho ametoa Vizimba vitano vya ufugaji wa Samaki kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Mara ili kusaidia jumuiya kujiimarisha kiuchumi.
Vizimba hivyo vitano ambavyo vitatumika kufugia samaki katika ziwa Victoria vina thamani ya shilingi Milioni 125.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya uongozi ya UWT mkoa wa Mara mjini Musoma June 18 mwaka huu 2026 dkt Nyansaho amesema lazima jumuiya hiyo muhimu ya chama cha Mapinduzi iweze kuimarika kiuchumi.
Waziri Nyansaho amesema kutokana na ukubwa wa Jumuiya hiyo inahitaji kuwa na mapato yake ili waweze kujitegemea katika uendeshaji wa shughuli zake na kujitegemea hasa nyakati za chaguzi.
Amesema Jumuiya hiyo ni miongoni mwa Jumuia kubwa na muhimu ndani ya CCM hivyo wataendelea kutafuta fursa mbalimbali za kiuchumi ili kukuza uchumi wa Jumuia, familia na Taifa kwa ujumla.
Sambamba na hilo Waziri huyo pia ameiahidi Jumuia hiyo kuwa atatafuta pesa kwaajili ya ujenzi wa nyumba za Watumishi wa Jumuiya hiyo ili kuweka mazingira bora na salama ya kiutendaji.
Ametumia fursa hiyo kuitaka Jumuiya hiyo kusimamia masuala ya malezi, maadili, msisitizo wa amani na utulivu ili kuwa na Taifa lenye kizazi bora na salama.
Naye katibu wa UWT Mkoa wa Mara, Sophia Maregesi amesema lengo la mafunzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu ni kuwajengea uwezo wanawake viongozi wa jumuiya hiyo ndani ya mkoa na wilaya zote ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Nancy Msafiri amesema katika mafunzo hayo, washiriki wamejifunza namna ya kutekeleza majukumu yao kwa tija'huku washiriki pia wakipewa jukumu la kuanza maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 na kuhakikisha chama kinaendelea kupata ushindi na kushika dola.










Comments
Post a Comment