Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mohamed Simai Said, amesema Watanzania wameelewa vyema kauli yake kuhusu Yuda aliyotoa bungeni, akisisitiza kuwa suala hilo ni la zamani na sasa anataka kuangazia utekelezaji wa bajeti na maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jun 23,2026 Bungeni Jijini Dodoma Simai amesema ni kawaida kwa wabunge kutofautiana na kukubaliana katika mijadala ya bunge, lakini mwisho wa siku wote hufanya kazi kwa lengo la kuwatumikia wananchi.
Amesema anaamini Watanzania ni watu wazima na wameitafsiri kwa usahihi kauli yake kuhusu Yuda, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kujadili suala hilo.
"Ninaamini Watanzania ni watu wazima na wameelewa nilichosema kuhusu Yuda. Jambo hilo lilishapita, na kama nilivyofundishwa shuleni, historia ni somo linalohusu mambo yaliyopita," amesema.
Simai aliongeza kuwa kwa sasa kipaumbele chake ni kusimamia utekelezaji wa bajeti, kumshauri Rais na Serikali, pamoja na kushiriki katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, amewataka Watanzania kuelekeza nguvu katika kujenga taifa na kuachana na mijadala ya mambo yaliyopita.


Comments
Post a Comment