Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia chama Cha ACT WAZALENDO kiza Mayeye, amesema uamuzi wake wa kuipigia kura ya "Ndiyo" Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 umetokana na kutanguliza maslahi ya wananchi, akisisitiza kuwa jukumu la mbunge wa upinzani si kupinga kila jambo linaloletwa na Serikali, bali kuchambua, kushauri na kukosoa pale inapohitajika.
Akizungumza leo Jun 23,2026 katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma baada ya Bunge kupitisha bajeti hiyo, Mayeye amesema si mara yake ya kwanza kuunga mkono bajeti, akieleza kuwa hata alipokuwa mbunge katika Bunge la mwaka 2015 hadi 2020 aliwahi kufanya hivyo kwa kuzingatia maslahi ya wananchi aliokuwa anawawakilisha.
"Kwa sababu mimi ni mpinzani, haimaanishi lazima nipinge kila kitu. Kazi yangu kama mbunge ni kuwatetea wananchi, kuishauri Serikali, kuielekeza na pale panapohitajika kuikosoa kwa lengo la kuboresha huduma na maendeleo," amesema.
Mayeye amesema katika mjadala wa bajeti alitoa mapendekezo kadhaa ya maboresho, ikiwemo kuishauri Serikali kuondoa baadhi ya kodi ambazo zinaweza kuwa mzigo kwa wananchi.
Ameeleza kuwa pamoja na mapungufu aliyoyaona, bajeti hiyo imebeba fursa na miradi yenye manufaa makubwa kwa wananchi wa Kigoma Kaskazini na Watanzania kwa ujumla, hivyo haoni sababu ya kuikataa bajeti yote kwa sababu ya maeneo machache yanayohitaji maboresho.
"Ukikataa bajeti yote, maana yake unakataa hata yale mazuri yatakayowanufaisha wananchi wako. Kilicho muhimu ni kuonyesha mapungufu, kuyatolea ushauri na Serikali iyafanyie kazi," amesema.
Mbunge huyo ameeleza kuwa ameridhishwa na kauli ya Waziri wa Fedha ya kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na wabunge, akisema hatua hiyo inaonesha Serikali imekuwa tayari kusikiliza hoja zenye maslahi kwa wananchi na kufanya marekebisho pale inapobidi.
kiza amesisitiza kuwa msimamo wake wa kupigia kura ya "Ndiyo" unatokana na dhamira ya kuona wananchi wanapata manufaa ya bajeti huku Serikali ikiendelea kuboresha maeneo yenye changamoto kupitia ushauri wa wabunge, badala ya kupinga kila jambo kwa misingi ya kisiasa.


Comments
Post a Comment