Waziri wa Afya, Mhe Mohammed Mchengerwa amesema kuwa magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza yamesababisha vifo kwa watoto wachanga kuanzia umri wa mwaka 1 hadi 5 zaidi ya elfu 12 kila mwaka huku ugonjwa wa kansa ukikatisha maisha ya watanzania zaidi ya elfu 43 kila mwaka.
Hayo amebainisha leo Juni 23, 2026 jijini Dar es Salaam katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa Kikanda wa PEN-Plus (ICPPA 2026), unaowakutanisha viongozi, watunga sera, wataalamu wa afya, watafiti, washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika na sehemu nyingine za dunia ambapo amesema magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza huchukua zaidi ya asilimia 20 kila mwaka katika mfuko wa bima wa NHIF.
Aidha, Waziri Mchengerwa amesema kuwa serikali imejipanga katika kujikinga na magonjwa hayo yasiyokuwa ya kuambukiza huku akimpongeza Rais Samia kwa kufanikisha kupeleka vifaa tiba mbalimbali katika vituo vya afya ili kusaidia kuwafikishia huduma bora ya afya wananchi.
Kwa upande wake mkurugenzi wa WHO kanda ya afrika, Dkt. Mohamed Janab amesema kuwa zaidi ya dola trilioni moja inapotea kila mwaka katika kupambana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza huku akisema kuwa hadi kufikia mwaka 2030 magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza yanakadiliwa kuwa namba moja Afrika.
Nae, Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt. Rahma Hingora amewataka mama na baba lishe nchini kuzingatia upishi wa chakula bora katika kufanikisha harakati za kujikinga na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.
Mkutano wa Kikanda wa PEN-Plus (ICPPA 2026) umejikita katika kujadili namna ya kuimarisha huduma za afya na kuongeza ushirikiano katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.
Kupitia jukwaa hilo, washiriki wamebadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora zinazotumika katika mataifa mbalimbali kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Mijadala na mawasilisho yaliyotolewa yameangazia umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma na kuendeleza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta hiyo.
Kwa Tanzania, kuwa mwenyeji wa mkutano huo kumedhihirisha nafasi yake kama kitovu muhimu cha majadiliano ya maendeleo barani Afrika. Aidha, mkutano huo umeipa nchi fursa ya kuonesha hatua zilizofikiwa katika sekta ya afya, huku ukiimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo wanaoshiriki katika juhudi za kuboresha afya na ustawi wa wananchi.



Comments
Post a Comment