NAIBU Spika wa Bunge, Daniel Sillo amesema Tamasha la Bunge Grand Bonanza 2026 limekuwa jukwaa muhimu la kutangaza utayari wa Tanzania kuandaa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 na kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika maandalizi yake.
Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa michezo mbalimbali katika bonanza hilo lililofanyika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, Mhe. Sillo amesema kaulimbiu ya "Pamoja AFCON, Tanzania Tuko Tayari" inalenga kuujulisha ulimwengu kuwa Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa, huku ikiwakaribisha wageni kutoka mataifa mbalimbali kupitia mabalozi waliopo nchini.
Amesisitiza kuwa Bunge linaipongeza Serikali kwa hatua za maandalizi ya AFCON 2027 na litaendelea kushirikiana nayo kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa, sambamba na kuacha urithi wa maendeleo kwa sekta ya michezo na uchumi wa nchi.
Mhe. Sillo pia amesema Bunge Grand Bonanza limeendelea kuwa chachu ya kuimarisha afya, mshikamano na ushirikiano kwa kuwakutanisha wabunge, mabalozi, watumishi wa Bunge, taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi, hali inayochochea umoja wa kitaifa kupitia michezo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo imejipanga kuwezesha wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na AFCON 2027 kwa kuendelea kutoa mitaji na huduma mbalimbali za kifedha.
Bunge Grand Bonanza 2026 limeandaliwa na Bunge kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku likidhaminiwa na CRDB Bank, likiwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha ushiriki wa Watanzania kuelekea AFCON 2027.

Comments
Post a Comment