Mbunge wa Misungwi mkoani Mwanza, Silvery Salvator ameainisha vipaumbele vya maendeleo ya jimbo hilo akisisitiza umuhimu wa sekta za maji, kilimo, barabara, afya, elimu pamoja na fursa zinazotokana na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Akizungumza kuhusu hali ya maendeleo ya jimbo hilo, Salvator amesema kipaumbele kikubwa kwa wananchi wa Misungwi ni upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema licha ya jimbo hilo kuwa na vyanzo vikubwa vya maji, bado baadhi ya maeneo yanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji.
Katika sekta ya kilimo, ameeleza kuwa Misungwi ina fursa kubwa ya uzalishaji kupitia mabonde na maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji, ambayo yanaweza kutumika kuzalisha mazao ya chakula na biashara kama mboga mboga, matunda na nafaka.
Amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji utaongeza tija na kuchochea uchumi wa wananchi.
Kuhusu miundombinu ya usafiri, Mbunge huyo amesema ujenzi na ukarabati wa barabara pamoja na madaraja ni muhimu katika kufungua shughuli za kiuchumi.
Ameeleza kuwa baadhi ya maeneo hukumbwa na mafuriko wakati wa masika, hali inayosababisha kukatika kwa mawasiliano na kuathiri usafirishaji wa mazao na huduma za kijamii.
Aidha, amegusia umuhimu wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), akisema ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi itakayorahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka vijijini kwenda masoko ya ndani na nje ya nchi, hivyo kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kimataifa.
Katika sekta ya elimu, Salvator amesisitiza kuboreshwa kwa miundombinu ya shule ikiwemo madarasa, nyumba za walimu na mazingira bora ya kujifunzia ili kuinua kiwango cha elimu na kuwapa wanafunzi fursa bora ya mafanikio.
Kuhusu sekta ya afya, amependekeza ongezeko la vituo vya afya na uboreshaji wa huduma katika maeneo ya vijijini, hatua itakayowezesha wananchi kupata huduma kwa ukaribu na kupunguza changamoto ya umbali mrefu kufuata matibabu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa miundombinu ya umeme katika vitongoji vilivyobaki, akieleza kuwa umeme ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi hususan katika kuchakata mazao na kuanzisha viwanda vidogo vidogo.
Sambamba na hayo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa utendaji kazi wake mahiri ambapo amesema kuwa anaimani naye Kwa asilimia mia Moja.
Pia amesema matumaini yake kuwa Bajeti Kuu ya Serikali itaendelea kuzingatia vipaumbele vya wananchi wa Misungwi, huku akisisitiza kuwa utekelezaji madhubuti ndio utakaotoa matokeo halisi ya maendeleo katika jimbo hilo














Comments
Post a Comment