Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Mfumo wa Sema na Rais Mwinyi (SNR) umechangia kupunguza urasimu, kuimarisha uwajibikaji wa watendaji wa Serikali na kujenga daraja la mawasiliano kati ya wananchi na Serikali yao.
Akizungumza katika mahojiano maalum ya kutathmini miaka mitano ya mfumo huo yaliyofanyika Ikulu, Zanzibar, amesema SNR imewawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko na maoni yao moja kwa moja na kupatiwa ufumbuzi kwa haraka na uwazi.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa mfumo huo unashughulikia changamoto za kijamii na kiutendaji, huku masuala ya kimahakama yakipaswa kufuata taratibu rasmi za kisheria, ikiwemo kukata rufaa pale mwananchi anapokuwa hajaridhishwa na hukumu. Katika kipindi cha miaka mitano, SNR imepokea malalamiko 22,521, ambapo 20,623, sawa na asilimia 91.6, yamepatiwa ufumbuzi.
Kwa mwaka 2026, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) imetunukiwa Tuzo ya Taasisi Bora, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdallah, Tuzo ya Kiongozi Bora wa SNR, na Khadija Mpemba wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Tuzo ya Afisa Bora wa SNR, kwa mchango wao katika kuimarisha utekelezaji wa mfumo huo.






Comments
Post a Comment