KAMATI ya Siasa ya Mkoa wa Mara, ikiongozwa na Marwa Mathayo, leo Juni 22, 2026, imefanya ziara ya ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi wa Chujio na Usambazaji wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Serengeti, wilayani Serengeti, kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo muhimu unaotarajiwa kuimarisha huduma ya maji kwa maelfu ya wananchi.
Akiongoza Kamati hiyo katika ukaguzi wa Mradi wa ujenzi wa chujio na usambazaji wa Maji wa Miji 28 Katika Mji wa Serengeti leo Jun 22, 2016 wilayani Serengeti Marwa Mathayo ambapo Kamati hiyo imedai kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi huo.
kamati ilipata maelezo kuhusu hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi, unaohusisha ujenzi wa chanzo cha maji, chujio la kisasa la kusafisha maji, mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 31 pamoja na ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhi maji lenye uwezo wa lita milioni mbili katika eneo la DDH.
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi MEGA Engineering Limited chini ya usimamizi wa Mkandarasi Mshauri WAPCOS Limited, na hadi sasa umefikia asilimia 74 ya utekelezaji. Kazi zilizobaki zinaendelea kwa kasi, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 10, 2026.
Kamati hiyo ya Siasa ilieleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi ubora uliokusudiwa, ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya maji safi na salama.
Mara baada ya kukamilika, mradi huo unatarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 160,000 wa Mji wa Serengeti, hatua itakayopunguza changamoto ya upatikanaji wa maji, kuboresha afya za wananchi, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuinua ustawi wa jamii.
Mradi wa Miji 28 ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora ya maji safi na salama, sambamba na kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya huduma za kijamii nchini.




Comments
Post a Comment