Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, ameunga mkono kwa asilimia 100 Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027, akiieleza kuwa ni bajeti ya maendeleo iliyolenga kukuza uchumi, kuongeza mapato ya ndani, kuimarisha huduma za jamii na kuwezesha makundi mbalimbali ya wananchi kiuchumi.
Akichangia Bajeti Kuu ya Serikali leo Bungeni jijini Dodoma, Dkt. Mahera alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake, pamoja na Waziri wa Fedha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa kuwasilisha bajeti aliyoieleza kuwa ya kimkakati na yenye kuzingatia mahitaji ya wananchi.
Katika mchango wake, Dkt. Mahera ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake, wazee na wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, akisema kundi hilo limeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa wananchi.
Ameishauri Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa machinga kwa kuwapatia maeneo rasmi ya kufanyia biashara, kuwawezesha kupata mitaji nafuu na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha shughuli zao ili waweze kukua kiuchumi na kuongeza mchango wao katika mapato ya taifa.
Aidha, amesema bajeti hiyo imeweka mkazo katika kuongeza mapato ya ndani, kuimarisha sekta ya kilimo na viwanda, kuboresha huduma za afya kupitia Bima ya Afya kwa Wote, kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuendeleza miradi ya maji, barabara na nishati.
Mbunge huyo pia ameishauri Serikali kutokusita kukopa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi, hususan ujenzi wa vituo vya afya na miundombinu mingine muhimu, akieleza kuwa mikopo inayokwenda kwenye uwekezaji wa maendeleo huongeza tija kwa taifa.
Vilevile, aliishauri Serikali kuiwezesha Bohari ya Dawa (MSD) kwa kuilipa madeni yake kwa wakati na kuiongezea uwezo wa kifedha ili iweze kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa muhimu za afya katika hospitali na vituo vya kutolea huduma nchini.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Dkt. Mahera aliipongeza Serikali kwa hatua za kulinda uzalishaji wa mafuta ya kula yanayotokana na alizeti nchini, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuweka sera zitakazowalinda wakulima wa alizeti na viwanda vya ndani ili kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini.
Kwa upande wa Jimbo la Butiama, aliiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, kutatua changamoto ya maji katika zaidi ya vijiji 20 na kuendelea kuboresha huduma za msingi kwa wananchi.
Dkt. Mahera amesema Bajeti Kuu ya Serikali imejibu matarajio ya wananchi na itaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo akaunga mkono hoja hiyo kwa asilimia 100.

Comments
Post a Comment