Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amewataka Waheshimiwa Wabunge kutumia majukwaa yao kuhamasisha wananchi, hususani waliojiajiri, kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili waweze kunufaika na huduma na mafao mbalimbali yanayotolewa na mifuko hiyo.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa makundi ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakishiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa, lakini bado hayajafikiwa ipasavyo na huduma za hifadhi ya jamii.
Bw. Mshomba ameeleza kuwa kuongezeka kwa wanachama katika mifuko ya hifadhi ya jamii kutasaidia juhudi za Serikali za kupunguza umaskini wa kipato, kuongeza tija katika uzalishaji mali, kukuza uchumi wa nchi na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 15, 2026, katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, wakati wa mafunzo maalumu kwa Waheshimiwa Wabunge yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Katika mafunzo hayo, wabunge walipatiwa elimu kuhusu mpango wa kuwajumuisha wananchi waliojiajiri katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuwawezesha kupata kinga ya kiuchumi na kijamii pamoja na mafao mbalimbali yanayotolewa na mifuko hiyo.
Akifafanua kuhusu walengwa wa SKIMU YA TAIFA YA HIFADHI YA JAMII KWA WANANCHI WALIOJIAJIRI, Mkurugenzi huyo amesema mpango huo unalenga wananchi waliojiajiri katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa, biashara za bodaboda, umachinga, pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Makundi mengine ni pamoja na wasusi, wachuuzi wa masokoni, mama lishe, baba lishe na wananchi wengine wanaofanya shughuli za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi.
Aidha, alibainisha kuwa ili mwananchi aweze kujiunga na skimu hiyo anatakiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 15 hadi 70, awe Mtanzania na mkazi wa Tanzania Bara, asiwe mnufaika wa mafao ya pensheni kutoka mfuko mwingine wa hifadhi ya jamii na awe anajishughulisha na shughuli za kujiajiri.
Bw. Mshomba amesisitiza kuwa ushiriki wa wabunge katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii utasaidia kujenga jamii yenye usalama wa kipato, ustawi wa maisha na uhakika wa maisha bora ya baadaye



Comments
Post a Comment