Serikali imesema itaendelea kushughulikia changamoto ya uhaba wa majosho katika Jimbo la Butiama, huku ikizitaka halmashauri nchini kutumia ipasavyo mapato yatokanayo na mifugo ili kuboresha huduma za afya ya mifugo kupitia ujenzi na ukarabati wa majosho.
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema Serikali inatambua mahitaji yaliyopo katika jimbo hilo na tayari imepokea barua rasmi iliyowasilishwa na mbunge huyo, ambayo itasaidia kutoa mwongozo katika utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya mifugo.
Waziri Kakurwa amempongeza Dkt. Mahera kwa kuibua na kufuatilia suala hilo kwa njia rasmi, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali, wabunge na mamlaka za serikali za mitaa ni muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji.
Amesisitiza kuwa majosho yana mchango mkubwa katika kudhibiti magonjwa ya mifugo, kuboresha afya ya wanyama na kuongeza uzalishaji, hivyo ni muhimu kwa halmashauri kuyapa kipaumbele katika mipango na matumizi ya mapato yatokanayo na sekta ya mifugo.
Aidha, Waziri huyo amewataka wabunge na madiwani kuendelea kuwa sauti ya wafugaji katika maeneo yao kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha uwekezaji katika miundombinu ya mifugo, hatua itakayosaidia kupunguza uhaba wa majosho na kuimarisha ustawi wa sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa wananchi.

Comments
Post a Comment