Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Devotha Minja, imekutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujadili taarifa ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2025, iliyokaguliwa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika kikao hicho, PAC imeitaka TRA kurekebisha mapungufu yote yaliyoainishwa na CAG, hususan katika maeneo ya ukusanyaji wa kodi na usimamizi wa mapato ya Serikali.
Aidha, Kamati hiyo imeielekeza TRA kuimarisha mifumo ya usimamizi wa kodi nchini kwa kuongeza ufanisi wa ukaguzi, uhakiki wa mapato na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa makusanyo ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema taasisi hiyo imepokea maelekezo yote ya Kamati na itayafanyia kazi ndani ya muda uliopangwa ili kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Uledi Mussa, amesema majadiliano hayo yamekuwa fursa muhimu ya kujifunza maeneo yenye changamoto na yanayohitaji kuongezewa nguvu na weledi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na walipa kodi.
Amesema lengo la TRA ni kuwa taasisi inayoaminika na wananchi, huku ikiendelea kuhamasisha utamaduni wa ulipaji kodi kwa hiari ili kupanua wigo wa mapato ya Serikali.
Pia ameomba PAC kuendelea kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya Taifa.






Comments
Post a Comment