KILIMANJARO INTERNATIONAL LEATHER INDUSTRIES CHATAJWA KUWA KIWANDA BORA CHA UZALISHAJI BIDHAA ZA NGOZI TANZANIA
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF), Bw. Fortunatus Makore Magambo, amewataka Waheshimiwa Wabunge kuwa mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini kwa kuzitumia na kuzitangaza, hatua itakayosaidia kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa taifa.
Akizungumza katika Ukumbi wa Msekwa leo Jun 15,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli na mafanikio ya Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited - KLICL), Bw. Magambo amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa bora za ngozi zinazoweza kushindana katika soko la kikanda na kimataifa kutokana na upatikanaji wa malighafi za kutosha na uwekezaji uliofanywa katika sekta hiyo.
Amesema KLICL, imeendelea kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa vya uchakataji wa ngozi nchini kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo viatu, mikanda, mabegi na bidhaa nyingine zinazokidhi viwango vya ubora vya kimataifa.
“Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge muwe mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa hapa nchini. Mkitumia na kuzitangaza, mtasaidia kujenga imani kwa wananchi na kuongeza soko la bidhaa zetu za ndani,” amesema Magambo.
Ameeleza kuwa matumizi makubwa ya bidhaa zinazozalishwa nchini yatasaidia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa hizo nje ya nchi.
Bw. Magambo amesema kiwanda hicho kinaendelea kutekeleza mkakati wa kupanua masoko yake ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha uwezo mkubwa wa uzalishaji uliowekezwa unatumika kikamilifu. Alitaja masoko yanayolengwa kuwa ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki na mataifa mengine kama China, Saudi Arabia, Italia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Misri, Pakistan na Uturuki.
Katika hatua inayoonyesha kuongezeka kwa ushindani wa bidhaa za ngozi za Tanzania katika soko la dunia, menejimenti ya KLICL ilieleza kuwa wanunuzi kutoka China tayari wameidhinisha sampuli za bidhaa zake, jambo linalotarajiwa kufungua fursa za oda kubwa zaidi katika siku zijazo.
Aidha, kiwanda hicho kimefanikiwa kuuza vipande 48 vya ngozi ya mbuzi kwenda China kwa thamani ya Dola za Marekani 15,000, hatua inayotajwa kuwa ishara ya kuimarika kwa mahitaji ya bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini katika masoko ya kimataifa.
Pamoja na mafanikio hayo, Magambo amesema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni upanuzi wa masoko ili kuendana na uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho, akisisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi, sekta binafsi na wananchi katika kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani ni muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda.
KLICL ni miongoni mwa viwanda vikubwa na vya kisasa zaidi vya uchakataji wa ngozi katika Afrika Mashariki na Kati, kikiwa na teknolojia ya kisasa inayowezesha uzalishaji wa bidhaa bora, imara na zinazokidhi viwango vya kimataifa. Kupitia uwekezaji huo, Tanzania inaendelea kupiga hatua katika kuongeza thamani ya rasilimali zake na kuifanya sekta ya ngozi kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa.





Comments
Post a Comment