Mbunge wa Kasulu Vijijini, Mhe. Edibilly Kazala, ametoa msisitizo kwa Serikali kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta za uzalishaji hususan kilimo na viwanda, akieleza kuwa ndiyo nguzo kuu za kupunguza umaskini na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Akichangia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 leo Juni 15, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Mhe. Kazala alianza kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake imara unaoendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi.
Pia amewapongeza Mawaziri pamoja na wataalam wa Wizara ya Fedha kwa kuendelea kuboresha mifumo ya kiuchumi na kuyafanyia kazi maoni ya Wabunge, akisema kuwa hatua hizo zimeleta mabadiliko chanya katika baadhi ya sekta muhimu.
Aidha, Mbunge huyo ameeleza kufurahishwa na juhudi za Serikali katika kulinda viwanda vya ndani, hususan sekta ya nguo (textile industry), akisisitiza kuwa sera hizo zimeanza kuleta matokeo chanya katika kuongeza thamani ya mazao ya ndani.
Hata hivyo, ameishauri Serikali kuongeza kasi zaidi ya mapambano dhidi ya umaskini kwa kuimarisha maeneo matatu makuu: kuongeza uzalishaji, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.
“Kama nchi tunapaswa kuhakikisha tunaimarisha uzalishaji, tunakusanya mapato kwa ufanisi na tunalinda kila shilingi inayopaswa kuingia serikalini. Hapo ndipo tutapata maendeleo ya kweli,” amesisitiza.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Kazala alisema bado mchango wake katika uchumi ni mkubwa lakini bajeti inayotengwa haiendani na umuhimu wake, akieleza kuwa sekta hiyo inaajiri zaidi ya asilimia kubwa ya Watanzania na inachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.
Amependekeza Serikali kuongeza bajeti ya kilimo kutoka kiwango cha sasa hadi kufikia angalau trilioni 3 hadi 4 ili kuongeza tija na uzalishaji, akisisitiza kuwa sekta hiyo ikipewa kipaumbele inaweza kuongeza mara dufu mapato ya taifa.
Kwa upande wa viwanda, amesema Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao badala ya kuuza malighafi nje ya nchi, akisisitiza umuhimu wa kuzuia uuzaji wa mazao ghafi kama pamba ili kuongeza ajira na mapato ya ndani.
“Ni muhimu tuendelee kuongeza thamani ya mazao yetu hapa nchini. Hii itatengeneza ajira nyingi na kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya uchumi wetu,” amesema
Katika eneo la uwezeshaji wananchi, Mbunge huyo amebainisha kuwa bado changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji ipo, hususan kwa vijana na wafanyabiashara wadogo.
Ameshauri kuwepo kwa mifumo rafiki ya upatikanaji wa mikopo ili kuwawezesha wananchi kuingia kwenye uzalishaji na kujiajiri kwa urahisi zaidi.
Aidha, amependekeza Serikali iangalie uwezekano wa kuwawezesha wahitimu wa vyuo vikuu kwa mitaji pindi wanapomaliza masomo yao, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.
“Vijana wetu wanapotoka vyuoni, wasibaki mitaani. Tuwawezeshe kwa mitaji hata ya kuanzia ili waanzishe shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa,” ameongeza.
Amesisitiza kuwa mustakabali wa uchumi wa Tanzania unategemea uwekezaji mkubwa katika sekta za uzalishaji, uimarishaji wa ukusanyaji wa mapato, na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya umma.

Comments
Post a Comment