Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imekutana na Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo tarehe 15 Juni 2026 jijini Dodoma kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Devota Minja, Kamati imeipongeza TRA kwa juhudi zake katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa walipakodi.
Sambamba na hilo, Kamati ilitoa maelekezo kwa TRA kuendelea kuimarisha mifumo yake ya kazi, kuongeza ufanisi pamoja na kuhakikisha utoaji wa taarifa za utekelezaji kila robo mwaka.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bw. Uledi Abbas Mussa, amesema Mamlaka itaendelea kuboresha mfumo wa kodi za ndani (IDRAS) kwa kutumia lugha nyepesi ya Kiswahili ili kurahisisha huduma kwa walipakodi.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, ameishukuru Kamati hiyo kwa kuendelea kutoa miongozo na kutumia nafasi hiyo kuijulisha Kamati kuwa maadhimisho ya miaka 30 ya TRA tangu kuanzishwa kwake yatafanyika Julai Mosi mwaka huu.








Comments
Post a Comment