Serikali imeweka mkazo katika kujenga uchumi himilivu unaotegemea mageuzi ya kidijitali, uwekezaji wa kimkakati na usimamizi madhubuti wa fedha za umma kupitia Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 inayolenga kuharakisha maendeleo jumuishi na kuongeza ustawi wa wananchi.
Akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar amesema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wengi wanaoishi vijijini pamoja na kundi kubwa la vijana, huku ikilenga kuimarisha uchumi wa wananchi na kupunguza tofauti za maendeleo kati ya mikoa.
Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya vijijini, kuendeleza mageuzi ya sekta ya kilimo, kuboresha huduma za jamii na kutekeleza mikakati maalumu ya kuinua uchumi wa maeneo yaliyobaki nyuma kimaendeleo.
Katika mwaka 2026/27, Serikali imejipangia kukuza uchumi kwa asilimia 6.3 kutoka asilimia 5.9 mwaka 2025, kuongeza mapato ya ndani kufikia asilimia 17.1 ya Pato la Taifa na kudhibiti mfumuko wa bei katika kiwango cha asilimia 3 hadi 5 ili kuendelea kulinda uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha.
Pia, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati yenye lengo la kuchochea uzalishaji, biashara na uwekezaji, ikiwemo uhuishaji wa reli ya TAZARA na ujenzi wa reli ya SGR, ambayo inatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa upande mwingine, Serikali imeeleza kuwa itaongeza kasi ya maendeleo ya viwanda vinavyotegemea rasilimali za madini na nishati, hususan gesi asilia, madini adimu, chuma na makaa ya mawe, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujenga uchumi mkubwa, wa kisasa na wenye ushindani.
Waziri Omar amesema utekelezaji wa malengo hayo utawezeshwa na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, ushiriki mkubwa wa sekta binafsi katika uwekezaji, utulivu wa bei za bidhaa na huduma, pamoja na kuendelea kuwepo kwa amani, usalama na utulivu nchini.

Comments
Post a Comment