Mbunge wa Jimbo la Mbogwe Mkoa wa Geita,Mhe Fagason Nkingwa,amesema ana matarajio makubwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/2027 inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni Juni 11, 2026, akieleza kuwa anatarajia bajeti hiyo kuleta majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Akizungumza nje ya viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Juni 10, 2026, Nkingwa amesema ana imani na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na namna ilivyokuwa ikisikiliza maoni ya wananchi na kuyajumuisha katika mipango ya maendeleo.
"Imani yangu kwa Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kubwa. Serikali hii imeendelea kuwa sikivu kwa wananchi wake, na sisi wabunge tumeshiriki kikamilifu kuchangia bajeti za wizara mbalimbali. Ninaamini bajeti itakayowasilishwa kesho itakuja na majibu ya changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja," amesema Nkingwa.
Nkingwa ametaja miundombinu ya barabara kuwa miongoni mwa maeneo anayotarajia kupewa uzito mkubwa katika bajeti hiyo, akibainisha kuwa wananchi wa Mbogwe na maeneo mengine nchini wanaendelea kukabiliwa na changamoto za usafiri na usafirishaji kutokana na hali ya baadhi ya barabara.
"Ninaamini Wizara ya Ujenzi itapewa fedha za kutosha ili kuimarisha mtandao wa barabara nchini. Hii itasaidia kufungua fursa za kiuchumi, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wananchi wa Mbogwe na Tanzania kwa ujumla," amesisitiza.
Mbunge huyo amesema bajeti zinazowasilishwa na wizara mbalimbali zimeonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo ana matarajio makubwa kuwa bajeti kuu itaimarisha sekta muhimu zinazochochea ustawi wa jamii na uchumi.
"Wananchi wanahitaji kuona matokeo ya maendeleo katika maeneo yao. Bajeti ya kesho inapaswa kuwa chachu ya kutatua changamoto zilizopo na kuendelea kujenga Tanzania yenye maendeleo jumuishi kwa kila mwananchi," amesema.
Amehimiza kwa kueleza kuwa matarajio yake ni kuona bajeti hiyo ikiweka mbele maslahi ya wananchi, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha huduma muhimu ambazo zinachangia ustawi wa Watanzania wote.


Comments
Post a Comment