Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Mhe. Kornel Magembe, amesema ana matarajio makubwa na Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27 inayotarajiwa kusomwa Juni 11, 2026, akieleza kuwa bajeti hiyo inapaswa kubeba na kutekeleza maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza kuhusu matarajio yake, Magembe amesema miundombinu ya barabara ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele ili kurahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya wananchi wa Chato Kaskazini.
Ametaja baadhi ya miradi ya barabara iliyopangwa kutekelezwa kupitia bajeti hiyo ikiwemo barabara ya Nyamirende–Biharamulo yenye urefu wa kilomita 50, pamoja na barabara ya Katende–Kachwamba–Kasenga inayotarajiwa kujengwa kupitia TARURA. Pia ametaja barabara ya kilomita 1.8 katika Kata ya Mgaza inayopangwa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mbunge huyo amesema kutokana na jiografia ya jimbo lake kuwa kandokando ya Ziwa Victoria, wananchi wanahitaji huduma bora za usafiri wa majini ikiwemo meli na boti za kusafirisha watu pamoja na mazao ya uvuvi kutoka maeneo hayo kwenda visiwani Ikuza na maeneo mengine ya visiwa vilivyopo katika ukanda huo.
Katika sekta ya afya, Magembe amesema bado kuna haja ya kuongeza uwekezaji ili kukamilisha vituo vya afya katika kata zote 14 za jimbo hilo. Amesema hadi sasa ni vituo vinne pekee vilivyokamilika na kujitosheleza kwa huduma muhimu, huku kata nyingine zikihitaji ukamilishaji wa majengo, vifaa tiba na watumishi wa afya.
Aidha, ameishauri Serikali kuendelea kuwekeza katika sekta ya mifugo kwa kujenga mabwawa na malambo ya maji yatakayosaidia kukabiliana na changamoto ya ukame inayozikumba kata za Ihamchale, Katende, Mkome na Kachwamba, hususan wakati wa kiangazi.
Kwa upande wa kilimo, Magembe amesema wananchi wa Chato Kaskazini wanatarajia kuona utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ili kuongeza tija na kuhamasisha kilimo cha kisasa. Ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa mipango ya kuanzisha mradi wa umwagiliaji utakaoanzia katika Kata Mbalimbali za chato kusini ikiwemo nyamirembe.
Magembe amesema wananchi wa Chato Kaskazini pamoja na wabunge kwa ujumla wanatarajia Bajeti ya 2026/27 kutekeleza kikamilifu ahadi za maendeleo zilizowekwa na Serikali pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ili kuendelea kuboresha maisha ya wananchi.

Comments
Post a Comment