Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini mkoani Geita, Paschal Lutandula, amesema Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27 inayotarajiwa kusomwa Juni 11, 2026, imebeba matumaini makubwa kwa wananchi wa jimbo hilo kutokana na miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha yao.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge leo Jun 10,2026 Jijini Dodoma, Mbunge wa Jimbo la chato kisini, Paschal Lutandula amesema moja ya vipaumbele vikubwa ni utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Buzilayombo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 23, pamoja na uchimbaji wa visima zaidi ya vitano vitakavyosaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.
"Baada ya mwaka wa fedha 2026/27, changamoto ya maji katika Jimbo la Chato Kusini itakuwa imepungua kwa kiwango kikubwa. Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji karibu na maeneo yao," amesema.
Katika sekta ya umeme, amesema Serikali inaendelea kukamilisha usambazaji wa huduma hiyo katika vitongoji vilivyosalia, huku vitongoji 52 vikitarajiwa kufikiwa na umeme ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Lutandula pia ameeleza kuwa maendeleo ya miundombinu ni miongoni mwa maeneo yatakayopata msukumo mkubwa kupitia bajeti hiyo.
Amesema mbali na fedha za Serikali, yeye binafsi ametoa mchango mkubwa kwa kununua mitambo ya ujenzi wa barabara yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.1, hatua ambayo tayari imeanza kuzaa matunda katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
"Nimetumia fedha kununua mitambo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ndani ya jimbo letu. Tayari kazi zimeanza na ukienda Bwanga leo utakuta barabara zinachongwa na kujengwa kwa kiwango kizuri. Hii ni hatua kubwa ambayo wananchi wameisubiri kwa muda mrefu," amesema.
Amefafanua kuwa uboreshaji wa barabara utarahisisha usafirishaji wa mazao, huduma za usafiri na biashara, jambo litakaloongeza kasi ya maendeleo ya uchumi wa wananchi wa Chato Kusini.
Kwa upande wa afya, mbunge huyo amesema mipango iliyopo katika bajeti hiyo ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika eneo la Bwanga, itakayopunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
Katika sekta ya elimu, amesema Serikali imepanga kuongeza vyumba vya madarasa, kujenga shule za sekondari na kuanzisha chuo cha VETA ili kuwapa vijana fursa zaidi za elimu na mafunzo ya ufundi.
"Hii ni bajeti inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Inaenda kuboresha maji, umeme, barabara, afya na elimu. Haya ndiyo maeneo yanayoleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu," amesema.
Lutandula amewataka wananchi wa Chato Kusini kuendelea kuwa na imani na Serikali, akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi iliyopangwa katika bajeti ya 2026/27 utaleta mabadiliko makubwa na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo katika jimbo hilo.
"Wananchi wa Chato Kusini waendelee kuwa na matumaini. Bajeti hii ina majibu ya changamoto nyingi na inaleta maendeleo makubwa tunayoyatarajia kwa muda mrefu," amesema.


Comments
Post a Comment